Uzalishaji wa mafuta ya visukuku waongezeka mwaka 2024 – DW – 13.11.2024

Wanasayansi hao wamesema hali hii inaongezeka huku kukiwa hakuna dalili yoyote ya wazi na ya dharura ya kudhibiti uchafuzi huo unaochochea ongezeko la joto duniani.

Uzalishaji wa hewa ukaa ulimwenguni umeendelea kuwa chanzo kikuu cha mabadiliko ya hali ya hewa na kulingana na wanasayansi hao ipo haja ya kuhakikisha uzalishaji huo unapungua kwa haraka hadi kiwango cha sifuri kama ulimwengu unanuia kupunguza ongezeko la joto linaloweza kuwa na athari kubwa.

Soma pia: Joto la 2023 halikuwahi kushuhudia miaka 100,000 iliyopita

Lakini tathmini ya karibuni ya bajeti ya kimataifa ya masuala ya uzalishaji wa kaboni ambayo huchapishwa kila mwaka inaonyesha uzalishaji wa hewa hiyo chafu kutokana na matumizi ya mafuta na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kama vile ukataji miti umeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2023, kwa jumla ya tani bilioni 41.6 kutoka tani bilioni 40.6 mwaka jana.

Tahadhari hii inatolewa wakati mataifa yakikutana mjini Baku, Azerbaijan kwa ajili ya duru ya karibuni ya mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa yanayojikita katika ufadhili kwa nchi maskini zaidi ili kuendeleza uchumi safi na kukabiliana na athari ambazo tayari haziepukiki za mabadiliko ya hali ya hewa na jinsi zinavyojitayarisha kuwasilisha mipango mipya ya utekelezaji wa 2035.

Matumizi ya mafuta ya visukuku huenda yakaongezeka kwa asilimia 0.8, 2024

Uzalishaji wa kaboni duniani kutokana na uchomaji na matumizi ya nishati ya kisukuku unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 0.8 mwaka 2024 kwa kufikia tani bilioni 37.4, hii ikiwa ni kulingana na Mradi wa Global Carbon, unaohusisha watafiti kote ulimwenguni.

Magari ya umeme
Baadhi ya magari yanayotumia umeme, ikiwa ni moja ya hatua zinazichukuliwa na mafaifa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaaPicha: PRAKASH MATHEMA/AFP

Ni ripoti inayotolewa licha ya hatua zilizopigwa za kusambaza vifaa mbadala na magari ya umeme, katikati ya ongezeko la matumizi ya gesi na mafuta, huku matumizi ya makaa ya mawe yakiongezeka kidogo. Ongezeko la uzalishaji wa mafuta ya kisukuku lilitokana na ongezeko la safari za ndege baada ya janga la UVIKO-19.

Soma pia:COP28 yafikia makubaliano kuachana na nishati za visukuku 

Wakati huo huo, uzalishaji unaotokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi pia umeongezeka kwa mwaka huu hadi tani bilioni 4.2 za hewa ukaa huku hali mbaya ya ukame ikizidisha uzalishaji wa hewa hiyo kutokana na ukataji miti na uchomaji moto misitu.

Profesa Pierre Friedlingstein aliyeongoza utafiti huo ameonya “muda unayoyoma wa kufikia malengo ya Mkataba wa Paris” sawasawa na alivyowaonya viongozi wa dunia katika mkutano wa COP29 kwamba ni lazima wapunguze kwa kasi uzalishaji wa mafuta ya kisukuku.

Na ili kukidhi ukomo huo wa cha nyuzi joto 1.5, utoaji wa hewa chafu utalazimika kupungua kutoka viwango vya sasa hadi sifuri kufikia mwishoni mwa miaka ya 2030, aliongeza.

Watafiti hao wameyataja mataifa 22, yakiwemo mengi ya Ulaya, Marekani na Uingereza, ambapo uzalishaji wa mafuta ya kisukuku umepungua katika muongo uliopita, hata katika wakati uchumi wao unakua.

Lakini Dr. Glen Peters wa Taasisi ya Kimataifa ya Tafiti za Hali ya Hewa iliyopo Oslo amesema uzalishaji wa kiwango cha kuu kabisa haujafikiwa, lakini unakaribia.

Soma pia:Je, ni nini maana ya upotoshaji kuhusu tabia nchi?

Related Posts