BAADA ya Karikoo Dabi ya wanaume iliyopigwa Oktoba 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar na Yanga kushinda bao 1-0 dhidi ya Simba, hatimaye leo inashuhudiwa ya upande wa wanawake kuanzia saa 10:00 jioni.
Msimu huu timu hizo zimekutana mara moja, Oktoba 2 kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii na Yanga Princess ilishinda kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare 1-1.
Timu hizo zinakutana baada ya mwezi mmoja, lakini Simba ikionekana kuwa bora zaidi ya Yanga kwani kwenye mechi tatu za Ligi Kuu Wanawake msimu huu imeshinda zote na Wananchi wakitoa sare zote.
Katika Ligi Kuu, Yanga Princess haijawahi kuifunga Simba katika misimu mitano na mara ya mwisho kushinda ni mwaka 2018 kwa bao 1-0 lililofungwa na Clara Luvanga aliyetimka Al Nassr ya Saudi Arabia.
Hata hivyo, rekodi za jumla zinaonyesha kwenye ligi, Yanga imeshinda mechi moja tu dhidi ya Simba, hivyo leo ina nafasi ya kuendelea kujiuliza.
Tangu msimu mwaka 2018, Yanga imekutana na Simba mara 12 lakini imeambulia ushindi mara moja tu huku mechi nane ikipoteza na kutoka sare tatu.
Huo ni mchezo muhimu kwa Simba ambayo ikishinda itaendelea kusalia kileleni ikiwa na pointi 12 huku Yanga kama itapata pointi tatu itatoka nafasi ya sita hadi tatu bora na pointi sita.
Simba hadi sasa ndiyo timu pekee iliyoshinda mechi zote tatu ikitoa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Mlandizi Queens, 3-1 dhidi ya Fountain Gate Princess na Ceasiaa Queens 4-1.
Licha ya Simba kushinda michezo yote lakini bado ina udhaifu eneo la beki ikiruhusu bao karibu kila mchezo.
Safu ya beki ya timu hiyo inaundwa na Doto Evarist na Violeth Nickolaus kwa mabeki wa kati na pembeni Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Ruth Ingosi.
Violeth tangu msimu uanze ameshuka kiwango licha ya Dotto kufanya kazi kubwa ya kusahihisha makosa ambayo yamekuwa yakitokea eneo la ulinzi hasa pale kati. Mabeki hao wamekuwa wazito kwenye kufanya maamuzi ya haraka na kupangua mashambulizi ya hatari.
Ukiachana na mabeki pia eneo la kiungo bado Simba haitengenezi nafasi nyingi kwa washambuliaji.
Hata hivyo, faida kubwa na utajiri wa timu hiyo ipo kwenye eneo la ushambuliaji na mawinga na wanacheza Asha Djafar na Elizabeth Wambui ambao wote wana kasi.
Mawinga hao wana uwezo wa kushambulia kwa kasi na faida kubwa kwa Wambui ana nguvu ya kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.
Eneo la ushambuliaji licha ya kumkosa Aisha Mnunka, timu hiyo ina washambuliaji hatari kama Jentrix Shikangwa, Asha Mwalala na Shelda Boniface ambao wote wamefunga.
Kwa upande wa Yanga, hadi sasa bado haijaonyesha makali kwenye ligi kwani michezo mitatu iliyocheza imeambulia pointi tatu.
Chini ya Kocha Edna Lema ‘Mourinho’ imekuwa ikiruhusu bao kwa kila mchezo na kufunga mabao machache. Kiufupi timu hiyo ina udhaifu maeneo ya beki na ushambuliaji kwa kuruhusu bao na kukosa wamaliziaji wazuri.
Mwanzoni mwa msimu kwenye mechi mbili za Ngao ya Jamii, Yanga ilionyesha kiwango bora hasa eneo la beki na Angela Chineneri na Igwe Uzoamaka walipokezana kwenye kukaba kwa muunganiko mzuri.
Lakini tangu ligi ianze mabeki hao wameruhusu mabao mawili dhidi ya Bunda Queens na Mashujaa Queens.
Kuanzia eneo la ulinzi na hata viungo wa timu hiyo wamekosa ubunifu wa kutengeneza nafasi za kuwapa urahisi washambuliaji kukwamisha mipira kambani.
Danai Bhobho, Agnes Pallangyo na Ajmuna Rebbeca ni wachezaji ambao wamekuwa wakianza kwenye eneo la kiungo lakini wakikosa muunganiko eneo hilo.
Bhobho akiwa na Simba alikuwa akitumika kama beki wa pembeni na chini ya Mourinho anayecheza eneo la kiungo baada ya Irene Kisisa kuwa nje kutokana na majeraha ya goti.
Licha ya kucheza lakini bado amekosa umakini wa kupitisha pasi kwa kiungo mshambuliaji ili kurahisisha kazi kwa washambuliaji.
Hadi sasa washambuliaji wa Yanga bado hawajafunga bao kwenye ligi ikiwa miongoni mwa eneo ambalo lina changamoto yake.
Mshambuliaji, Ariet Udong ambaye ana sifa tatu za kuwa straika yaani kasi, nguvu na akili akikosa usaidizi wa viungo washambuliaji.
Kwenye mechi hizo alikuwa miongoni mwa wachezaji hatari lakini anapofika langoni anapata wakati mgumu wa kutoa pasi kwa kuwa viungo wake wanakuwa chini na kusindikiza mpira moja kwa moja.
Kocha wa Simba, Yussif Basigi alisema wanaingia kwenye mchezo huo bila ya kutazama matokeo ya nyuma yalikuwaje.
“Tunafahamu ni mchezo mgumu wa dabi, hivyo maandalizi tuliyofanya tunaamini tunakwenda kuchukua pointi tatu muhimu na kuendelea kusalia kileleni,” alisema Basigi.
Kocha wa Yanga, Edna Lema ‘Mourinho’ alisema anawafahamu wapinzani wake ni moja ya timu bora na wanapokutana inakuwa mechi ngumu.
“Mchezo uliopita tulishinda lakini hatuangalii matokeo yaliyopita, bali tunauendeaje mchezo wa ligi ambao unahitaji kupata pointi tatu na tunaamini tutashinda ingawa haitakuwa rahisi,” alisema.