Kwanini Moallin Yanga! KMC watoa tamko

YANGA wapo katika kipindi cha  kujiimarisha ili kurudi kwenye mstari baada ya kushuhudia michezo miwili iliyopita ikipoteza mfululizo nyumbani. Kabla ya hapo, timu hiyo haikuwahi kupoteza nyumbani katika mechi 50 mfululizo za ligi.

Rekodi hiyo ilianza kuvunjwa na Azam iliposhinda 1-0, kisha ikapokea kipigo cha aibu cha mabao 3-1 kutoka kwa Tabora United ambao walipigilia msumari wa matokeo mabaya kwa vijana hao wa Kocha Miguel Gamondi.

Kupoteza mechi hizo mbili za Ligi Kuu Bara ambapo ilikuwa mara ya kwanza kwao msimu huu baada ya kushinda mechi nane mfululizo tena bila ya kuruhusu bao, kimewatikisa kidogo vigogo hao ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo.

Kutikiswa huko kumewafanya kuchukua uamuzi mgumu huku taarifa zikielezwa kwamba wamemalizana na Kocha Abdihamid Moallin raia wa Marekani mwenye asili ya Somalia.

Moallin ambaye alikuwa akiinoa KMC, tayari ameaga ndani ya kikosi hicho huku uelekeo wake ukiwa ni Yanga kwenda kuchukua nafasi ya kocha msaidizi, Moussa N’Daw raia wa Senegal.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya Yanga, Moallin, aliyezaliwa Juni 9, 1989 (miaka 35) mwenye Leseni A ya CAF amekubali ofa hiyo na atakuwa sehemu ya benchi la ufundi la kikosi cha kwanza cha Yanga.

Majukumu hayo yatakuwa kama ilivyokuwa kwa Moussa Nd’aw aliyekuwa msaidizi wa Miguel Gamondi pia akihusika na timu za vijana.

“Tayari Moallin amekubaliana na Yanga kuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo na muda wowote anaweza kutambulishwa kwa sababu makubaliano yalikwenda vizuri.

“Moallin ana sifa zote za kuwa kocha mkuu. Kuwa naye ni hatua muhimu, hasa kipindi hiki ambacho mabosi wa Yanga wanapanga kuachana na Gamondi. Mnaweza kushangaa timu itakuwa chini yake kwa muda, wakati mchakato wa kutafuta kocha mpya ukiendelea. Lolote linaweza kutokea,” kilisema chanzo.

Kwa nini Moallin Yanga? inawezekana likawa swali ambalo pengine hata wewe likawa kichwani mwako lakini hizi hapa ni sababu zinazoelezwa zimechochea mabosi wa timu hiyo kumvuta fasta Jangwani.

Moallin amezoea mazingira ya soka la Tanzania kwa kufanya kazi na klabu kama Azam FC na KMC. Akiwa Azam alikorithi mikoba ya George Lwamdanina, alijifunza mikakati na mifumo ya uchezaji inayotumiwa kwenye ligi ya Tanzania na kuifanya timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu 2021/22, nyuma ya Simba na Yanga lakini bahati mbaya kwake msimu uliofuata alifutwa kazi baada ya michezo miwili tu ya ligi.

Kocha huyo mwenye uraia wa Marekani, awali alitua Azam Julai, 2021 akitokea Horseed SC ya Somalia na kuachana na timu hiyo Agosti 2022 akihudumu kwa msimu mmoja huku ule mwingine akiondoka mapema.

Baada ya kuachana na Azam, akakaa kwa muda kabla ya kuibukia KMC msimu wa 2023/24 na timu hiyo ilimaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Kwa kuongoza KMC, Moallin ameona changamoto na ushindani wa timu za kiwango cha kati dhidi ya klabu kubwa kama Yanga na Simba.

Uelewa huu unamwezesha kubaini nguvu na udhaifu wa wapinzani wa Yanga, jambo linalomsaidia kubuni mikakati inayowawezesha Yanga kutimiza malengo yao kwenye mashindano ya ndani na kimataifa.

Yanga kwa sasa iko kwenye mchakato wa kumtafuta kocha mkuu mpya, hivyo uwepo wa Moallin kwenye benchi la ufundi unawapa chaguo thabiti la muda mfupi au hata la kudumu, kulingana na mahitaji.  Moallin ana uwezo wa kusimamia kikosi endapo itahitajika, hasa wakati wa kipindi cha mpito.

Uwezo wake wa kufanya kazi kama kocha mkuu na katika nafasi za benchi la ufundi unaipa Yanga uhakika wa mtu anayeweza kumudu majukumu hayo.

Moallin ni kocha anayejulikana kwa kujenga nidhamu na kuhakikisha maadili miongoni mwa wachezaji wake ndani na nje ya uwanja, na kuwajibika katika majukumu yao.

Nidhamu hii huongeza viwango vya uchezaji na kuimarisha mshikamano wa timu, jambo ambalo ni muhimu kwa klabu kama Yanga.

Pia, nidhamu inayojengwa na Moallin itasaidia kudumisha utulivu kwenye klabu na kuweka msingi mzuri wa mafanikio ya muda mrefu, lakini kwake atapata uzoefu mkubwa kutokana na ukubwa wa Yanga.

Moallin anatambulika kwa mbinu za kisasa za kufundisha soka safi la kuvutia huku timu yake ikishambulia kuanzia nyuma, pia amekuwa akitilia mkazo matumizi ya teknolojia na ubunifu katika mazoezi na ushauri wa kiufundi.

Yanga, ikiwa na maono ya kuwa klabu ya kiwango cha kimataifa, itanufaika na mtazamo huu wa kisasa.

Teknolojia kama mifumo ya kufuatilia utendaji wa wachezaji, uchambuzi wa video, na takwimu za kisasa itasaidia klabu hiyo kuboresha mafunzo yao na kuwapima wachezaji kwa kina, jambo linalohitajika sana katika soka la kisasa.

Wakati Moallin akitajwa kumalizana na Yanga, uongozi wa KMC kupitia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Songoro Mnyonge amesema kocha huyo namna alivyoondoka ni kama ametoroka kazini kwani bado wana mkataba naye wa mwaka mmoja.

Songoro amebainisha kwamba, katika mkataba huo, unamtaka Moallin kama anataka kuondoka basi aandike barua ya mwezi mmoja kabla, hivyo kuondoka ghafla inawalazimu bodi kukaa kujadili namna ya kufanya kulifikisha suala hilo katika mamlaka husika kwa maana ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili wapate haki yao.

Miongoni mwa makocha waliowahi kufanya kazi na Moallin ni Mohammed Badru na anamzungumzia kwa kusema: 

“Ni kocha mwenye mtazamo wa kisasa, licha ya kuwa na umri mdogo, ana uwezo mzuri wa kufundisha mpira wa kisasa. Najua ubora wake wa kutumia vijana kwa sababu nimefanya naye kazi kwa karibu. Yanga, kama kweli imemalizana naye, inaweza kunufaika naye kwa miaka michache ijayo ikiwa atapewa uwanja mpana wa kufanya kazi.”

Moallin ameiongoza KMC ambayo ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi msimu huu kuvuna pointi 14 katika michezo 11.

YANGA WAPO SAWA KUHAMIA KMC

Wakati Yanga ikitangaza kuhamia KMC Complex kutoka Azam Complex, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa tamko. Awali wakati Yanga ikitangaza kuhama uwanja, Bodi ya Ligi ilibainisha imepokea ombi lao lakini haijalitolea uamuzi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda alisema Kanuni ya 9(4) inawapa haki Yanga na timu nyingine ambazo hazina uwanja wake inaoumiliki kuhama kama tu hawakuwa na makubaliano na wamiliki.

“Ni sawa kwa Yanga kuhama kwani makubaliano yao na Azam yameharibika, japo hatujawapa barua ya kibali ila kikanuni wanaruhusiwa kuhamia uwanja mwingine uliopo ndani ya mkoa huohuo au nje kidogo.

“Uwanja watakaohamia uwe umehakikiwa na Bodi ya Ligi kama utafaa kutumika, kwa hivyo ombi lao lina mashiko,” alisema Boimanda.

Related Posts