Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimelaani tukio la Katibu wake, Wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa, Christina Kibiki kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Christina ameuawa usiku wa kuamkia leo Jumatano Novemba 13, 2024, Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, wilayani Iringa alipokuwa akiishi. Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga lakini alifariki dunia.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilolo, John Kiteve, akizungumza na Mwananchi amesema tukio hilo la kusikitisha lilitokea kati ya saa 4:30 na 5:00 usiku wa kuamkia leo.
Taarifa kwa umma, iliyotolewa leo Jumatano na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla imeeleza, “Chama cha Mapinduzi, kimepokea kwa mshtuko mkubwa, taarifa za kifo cha Christina.
Makalla amesema marehemu alikuwa anajiandaa kuhudhuria semina elekezi kwa makatibu mjini Dodoma kesho Alhamisi, Novemba 14, 2024.
“Chama Cha Mapinduzi kinatoa pole kwa familia, ndugu, viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa kufuatia kifo cha ghafla na cha kikatili,” amesema Makalla na kuongeza:
“Tunawaomba wanachama wetu wawe watulivu wakati vyombo vya dola vikifuatilia na kuchunguza tukio hili, ili wahusika waweze kufikishwa katika vyombo vya kisheria.”
Juhudi za kuitafuta Polisi Mkoa wa Iringa kuzungumzia tukio hilo bado zinaendelea.
Endelea kufuatilia Mwananchi