Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbess Lema amewataka wanachama Mkoa wa Kilimanjaro kuvunja makundi ili kukipigania chama hicho na kukivusha hatua moja kwenda nyingine.
Lema amesema hayo alipozungumza kwenye mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika jana Jumanne Novemba 12, 2024.
Amesema ni vyema wakajifunza hawataweza kukivusha chama hicho kwa kutafuta vyeo.
“Nataka tujifunze, hatuwezi kukivusha chama hiki kwa kutafuta vyeo, hatuwezi, mimi kila mara natubu dhambi. Kuna watu tuliwaaminisha tunaamini katika haki, wakaenda kwenye maandamano mbele, wameuawa kwa sababu tuliwaambia twendeni, kama tukiishi maisha ya kukosa uadilifu ndani yetu, laana ya zile damu tujue ziko juu yetu,” amesema Lema.
Lema amewataka wanachama wa chama hicho kupendana ili kuepuka kuumizana wenyewe kwa wenyewe, hali inayosababishwa na wengine kukata tamaa na kurudi nyuma.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro aliyemaliza muda wake, Michael Kilawila amewataka wanachama kuepuka kuumizana badala yake waelekeze silaha zote kwa adui.
“Kila mtu alikuja na fito yake akajenga hii nyumba inayoitwa Chadema, ithamini hiyo fito moja, mbili au tatu ulizokuja nazo badala ya kumuumiza mwenzako kwa sababu ambazo hazina msingi, chama chetu tusikiingize katika majungu ya kulaumiana sisi wenyewe kwa wenyewe.
“Jeshi ambalo huwa linashindwa ni lile wanajeshi wanageuziana mitutu ya bunduki na kuanza kuuana wenyewe kwa wenyewe, rai yangu silaha zetu zote zielekezwe kwa adui yetu ambaye ni Chama cha Mapinduzi (CCM).”
Pia, amewataka viongozi waliopo na watakaochaguliwa, kwenda kutengeneza Serikali za vijiji katika maeneo yao.
“Rai yangu kwenu viongozi mliopo na mtakaochaguliwa, nendeni mkatengeneze Serikali za vijiji kupitia vyama vyenu, maana yake hata kama mwenyekiti wako aliyekuwa anagombea hakuteuliwa nendeni mkatengeneze Serikali yenu ya kijiji,” amesema.
Katika uchaguzi huo, Gervas Mgonja amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, akichukua nafasi ya Michael Kilawila ambaye hakugombea na anatajwa kwenda kugombea Kanda.
Mgonja alishinda baada ya kupata kura 47 dhidi ya wapinzani wake, Jornas Kadege aliyepata kura 34 na Collins Mayuta kura 12.
Kwa upande wa nafasi ya katibu, Basil Lema ameshinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 68 dhidi ya Antony Ndewawio aliyepata kura 24, huku Baraza la Wanawake (Bawacha), Grace Kiwelu akitetea nafasi yake ya uenyekiti na katibu akichaguliwa Sharifa Malya.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Mgonja aliwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumpatia nafasi ya kukiongoza chama hicho huku akiomba ushirikiano ili kuyafikia malengo ya kukivusha chama chao ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Basil ambaye amekuwa katibu wa chama hicho kwa muda sasa, amewashukuru wajumbe kwa kuendelea kumuamini na kuwataka kuungana kuchapa kazi.
“Niwashukuru wajumbe kwa kuniamini tena na tena, sasa tukachape kazi, najipanga kutembelea majimbo yote kuimarisha chama,” amesema.