Na Jane Edward, Arusha
Sheikh Hussein Said Junje, Sheikh wa Wilaya ya Arusha Mjini amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mhe. Paul Christian Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akimsifu kwa Uwajibikaji wake katika kusimamia haki za wananchi wa Arusha.
Sheikh Junje ametoa kauli hiyo Ofisini kwake Mjini Arusha wakati akizungumzia programu maalum ya Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha ya kutenga siku tatu Maalum za kusikiliza na Kutatua kero za wananchi ambazo zitakuwa Jumatano, alhamisi na Ijumaa ya Wiki hii.
Sheikh Junje amemtaja Mhe.Mkuu wa Mkoa Paul Christian Makonda kama kiongozi mwenye kuzingatia Kanuni zinazotokana na Quran na Sunnah za Mtume (SAW) ambazo ni Haki, Mashauriano, wajibu, Unyenyekevu na Huruma, akisema anayoyafanya Mhe. Mkuu wa Mkoa yanampendeza Muumba wetu aliyeumba pia Mbingu na Ardhi.
Ikumbukwe kuwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda amewaalika wananchi wote wa Arusha wenye changamoto na kero mbalimbali kufika ofisini kwake tarehe 8-10 Mei, 2024 ili kuweza kusikilizwa na kutatuliwa changmoto walizonazo huku Mkuu wa Mkoa akiahidi kujiandaa vya kutosha yeye na wasaidizi wake ili kuweza kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kama yalivyo Maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.