Lawrence Mafuru: Kielelezo cha nidhamu ya utaalamu katika utumishi wa umma

Nilianza kumsikia Lawrence Mafuru miaka ya 2010 pale alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC).

Katika umri wake wa miaka 40 wakati huo, uteuzi wake kuiongoza taasisi kubwa kama hii ulifanya watu wengi wamfuatilie, hususani ukizingatia alikuwa Mtanzania wa kwanza kupata fursa hiyo.

Niliendelea kumfuatilia Lawrence zaidi alipoteuliwa kuwa Msajili wa Hazina mwaka 2015, na mtazamo wake kuhusu uendeshaji wa mashirika ya umma.

Kupitia kauli alizotoa katika mihadhara mbalimbali ni wazi kuwa alikuwa na mipango mikubwa ya kubadili taswira ya mashirika ya umma na kuwa sehemu muhimu katika kuchangia maendeleo ya uchumi nchini.

Nilipata nafasi ya kuwa karibu na Lawrence mwaka 2021 baada ya mimi kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji). Niliandika makala katika Gazeti la The Citizen yenye kichwa cha habari “It is new dawn for investors in Tanzania (mwelekeo mpya kwa wawekezaji Tanzania).

Katika makala hii nilieleza mwelekeo mpya kwa wawekezaji nchini nikisisitiza kuwa Serikali itaipa nafasi kubwa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi nchini.

Makala hii iliibua hisia na matumaini makubwa kwa wawekezaji na wafuatilia wa masuala ya uchumi wa Tanzania kutokana na ukweli kwamba, katika miaka mitano ya mwanzo ya utawala wa Rais Magufuli mazingira ya uwekezaji yaliyumba.

Hivyo, wasomaji wa makala hii waliona pengine kulikuwa na mwelekeo tofauti chanya. Moja ya watu waliosoma makala hii kwa msisimko alikuwa Lawrence Mafuru, wakati huo akiwa katika taasisi yao iitwayo Bankable.

Baada ya kusoma makala hiyo yeye na wenzake walinitafuta na kupanga kuonana nao, nami nikawatembelea ofisini kwao. Walinieleza kufurahishwa na mwelekeo mpya wa Serikali na wangetaka tushirikiane na taasisi yao ya Bankable katika kuendelea kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji.

Kuanzia wakati huo nikawa karibu na Lawrence akiwa mshauri wangu wa kujitolea katika masuala ya uwekezaji. Kwa kweli, alinisaidia sana kwani alikuwa ananipa uchambuzi wa jinsi uwekezaji unavyokwenda duniani na nafasi ya Tanzania.

Julai 5, 2023 tuliteuliwa wote na Rais Samia Suluhu Hassan, yeye akiwa ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango na mimi nikiteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Tume yake ikiwa chini ya ofisi yangu.

Tulipokutana siku ya uapisho Julai 14, 2023 Ikulu, Dar es Salaam, tukataniana kwa maneno ya Kiingereza kuwa “what a sweet coincidence.” Nikamwelekeza kuwa sasa unakuwa rasmi mshauri wangu, siyo wa kujitolea tena!

Katika ziara yake ya kwanza ya kunitembelea ofisini baada ya kuapa, Lawrence aliniletea kitabu maarufu cha tasnia ya Lee Kuan Yew, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Singapore, kiitwacho “Lee Kuan Yew: The Man and His Ideas”.

Tukakubaliana kuwa nikisome kitabu hiki na tukikutana tuone namna mawazo yaliyomo humu yanavyoweza kusaidia katika mipango yetu. Nilipata kukisoma kitabu hiki miaka kadhaa iliyopita lakini niliamua kukisoma tena.

Ni kitabu muhimu sana kwa mtu yeyote anayefanya kazi katika taasisi ya umma inayohusika na mipango na uchumi wa nchi. Kupitia maudhui ya kitabu hiki na vingine tulibadilisha muundo wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka mmoja ambao huandikwa na Serikali kila mwaka.

Ukifuatilia utaona muundo na maudhui ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa mwaka 2023/2024, 2024/2025 na 2025/2026 yanatofautiana kwa kiasi fulani na mipango ya nyuma. Yote hii ni kwa sababu Lawrence aliamua tuboresha zaidi.

Tulikubaliana pia kuweka utaratibu wa kununua jarida la Harvard Business Review kila mwezi kwa lengo la kujua uchumi wa dunia unavyokwenda na kupata mawazo ya uongozi na jinsi ya kuendesha taasisi kwa mafanikio makubwa.

Kwa kiasi kikubwa Lawrence alikuwa anaijenga Tume ya Mipango iwe taasisi ya kimataifa kwa kuzingatia mawazo mengine kutoka Jarida la Harvard Business Review na majarida mengine ya kimataifa.

Kutokana na tabia yake ya kusoma na kujifunza mambo mengi duniani, Lawrence alikuwa mpana wa maarifa na hakufungwa na eneo moja la utaalamu.

Pamoja na kwamba hakusomea uchumi kama taaluma yake ya ubobezi, Lawrence alikuwa na taarifa nyingi kuhusu masuala ya uchumi duniani na Tanzania.

Ni yeye aliyetoa muhtasari mfupi kabisa wa changamoto za kiuchumi Tanzania mwaka 2023 wakati tukiandaa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2023/2024 pale alipoeleza kuwa uchumi wa Tanzania umekua vizuri kwa miaka yote 20 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Hata hivyo, changamoto kubwa ni ukweli kwamba, ukuaji huu umekuwa siyo jumuishi kwa kuwa sekta zinazokua siyo zile ambazo zinaajiri watu wengi.

Kwa kuzingatia hili, Dira ijayo ya Taifa ya Maendeleo imebeba neno ‘jumuishi’ kama sehemu muhimu sana ya maudhui.

Kutokana na uzoefu na upana wa maarifa aliyokuwa nayo, Lawrence alikuwa mshauri muhimu katika kazi yangu kama waziri mwenye dhamana ya mipango.

Ni mtumishi aliyekuwa na nidhamu ya utalaamu, na ushauri wake wote ulizingatia misingi ya sayansi ya jambo husika.

Lawrence aliweka wazi kuwa kutumia busara ni jukumu la viongozi na kwamba, ushauri wa wataalamu unapaswa kuzingatia sayansi na utaalamu na si busara na kwamba, kiongozi anapaswa kuambiwa ukweli wote wa jambo husika ili afanye uamuzi sahihi.

Lawrence aliugua muda mfupi. Katikati ya Agosti alienda Hospitali ya Taifa Muhimbili kupimwa zaidi. Tukiwa tunahudhuria mkutano wa wakuu wa taasisi za umma jijini Arusha Agosti 27, 2024 alituaga kuwa ameitwa ghafla afike hospitali kuchukua majibu yake.

Alipofika Muhimbili hakuruhusiwa kuondoka kutokana na hali ya vipimo ilivyoonyesha. Agosti 29, 2024 nilipigiwa simu kuwa hali ya Lawrence haikuwa nzuri, nikakimbia kwenda kumuona katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.

Madaktari wa Muhimbili waliamua Lawrence aende India kwa uchunguzi na matibabu zaidi. Agosti 31, 2024 tulisafiri pamoja, yeye akiwa anaelekea India kwa matibabu na mimi nikielekea China kuhudhuria mkutanao wa wakuu wa nchi za Afrika na China, nikiwa sehemu ya msafara wa Rais Samia.

Akiwa India tuliendelea kuwasiliana na matibabu yalikuwa yanakwenda vizuri kwa kiwango ambacho alishiriki kufanya kazi za Tume na Dira kwa njia ya mtandao.

Hata hivyo, wiki moja kabla ya kufikwa na umauti Lawrence hali yake ya afya ilibadilika sana. Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Lawrence Mafuru na mchango alioutoa katika familia na Taifa.

Nidhamu yake ya utaalamu iwe chachu kwa watumishi wa umma katika kuongeza bidii na kuboresha utumishi wao. Wosia mmoja muhimu kwa watumishi wa umma kutokana na maisha ya kiutumishi ya Lawrence ni kwamba, ni muhimu kwa watumishi wetu kujenga ujasiri wa kitaalamu ili wanaposhauri viongozi wazingatie ushahidi wa kisayansi.

Tunaendelea kumuomba Mungu ailaze roho ya marehemu Lawrence Mafuru mahala pema peponi. Amina

Kitila Mkumbo ni Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) na ambaye alifanya kazi kwa karibu na Lawrence Mafuru.

Mafuru alifariki dunia Novemba 9, 2024 akiwa anapatiwa matibabu nchini India.

Leo Jumatano, Novemba 13 maombolezo yanaendelea nyumbani kwa marehemu Bunju A.

Kesho Alhamisi Novemba 14, mwili wa Mafuru utaagwa katika ukumbi wa Karimjee kuanzia asubuhi, kisha utapelekwa nyumbani kwake utakapolala kabla ya shughuli za mazishi Ijumaa Novemba 15 katika makaburi ya Kondo, Tegeta jijini Dar es Salaam.

Related Posts