Najim, mkewe wafikisha siku 320 gerezani bila upelelezi kukamilika

Dar es Salaam. Mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya kusafirisha kilo 3,050 za dawa za kulevya, Najim Mohamed (52) na mkewe Maryam Najim (50) pamoja na  mfanyakazi wa ndani wa kiume, Juma Abbas (37), wamefikisha siku 320, wakiwa gerezani bila upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Washitakiwa hao wanaendelea kusota rumande kutokana na mashitaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mohamed na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu yenye mashitaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu.

Kwa mara ya kwanza, washitakiwa hao walifikishwa mahakamani Desemba 29, 2023 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka mawili.

Hata hivyo, tangu siku hiyo, hadi leo Novemba 13, 2024,  kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, washitakiwa hao wamefikisha siku 320, sawa na miezi 10 na siku 15 wakiwa mahabusu, kutokana na upelelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Awali, Wakili wa Serikali, Frank Rimoy aliieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea hivyo, wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia umefikia wapi,” amedai Rimoy.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lyamuya alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2024 itakapotajwa.

Hata hivyo, kesi hiyo ilisikilizwa kwa njia ya video huku washitakiwa hao wakiwa rumande.

Related Posts