ACT-Wazalendo, Chadema yataka uwajibikaji watendaji waliowaengua wagombea wao

Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa akiagiza kamati za rufani za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa ili kujiridhisha na sababu za kutoteuliwa, vyama vya ACT-Wazalendo na Chadema vimetaka uwajibika kwa watendaji walioengua wagombea wao kinyume cha utaratibu.

Vyama hivyo, vimetaka watendaji hao (wasimamizi wa uchaguzi) watakaokabainika waliowaengua wagombea uonevu wachukuliwe hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwa watumishi wengine.

Jana Jumanne Novemba 10, 2024 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mchengerwa alitoa maagizo kwa  kamati za rufani zinazoongozwa na makatibu tawala wa wilaya kuongeza muda wa siku mbili kupitia rufaa za wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

“Ninaelekeza kamati za rufani za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa ili kufanya mapitio na kujiridhisha na sababu zilizosababisha wagombea kutoteuliwa ili haki kutendeka kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi,” amesema Mchengerwa.

Msingi wa uamuzi huo wa Tamisemi ulitokana na kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliyeitaka Tamisemi kuyapuuza makosa madogo yaliyojitokeza wakati kwa wagombea wakati wa ujazaji wa fomu za kuwania uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika Novemba 27,2024.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Jumatano Novemba 11,2024 Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, alisema,“tunataka kuona hatua za kinidhamu zikichukuliwa kwa watendaji wote wa Tamisemi waliowaengua wagombea wetu kwa uonevu na ubaguzi, haitoshi tu wagombea kurejeshwa bali lazima kuwepo na uwajibikaji.”

Ado amesema pamoja na nia njema ya kuhakikisha demokrasia inastawi kufuatia maelekezo yaliyotololewa, lakini ACT-Wazalendo hairidhiki na mtindo wa kufanya kazi kwenye mambo ya msingi kwa kusubiri utashi wa maelekezo, wakati uchaguzi ni mchakato wa kisheria na kikanuni na sio hisani.

“Tanzania lazima itoke sasa kwenye demokrasia ya kupewa na badala yake tujenge demokrasia iliyosimikwa kwenye misingi ya kikatiba, sharia na kanuni, demokrasia ya maelekezo ndiyo imetufikisha hapa tulipo na lazima tutoke hapa, miaka zaidi ya 30 tangu mfumo wa vyama vingi kuanza,” amesema Ado.

Ado amesema chama hicho, kinaitaka Tamisemi kuwarejesha wagombea wao waliondolewa kwa sababu ya ngazi mbalimbali ikiwamo udhamini warejeshwe.

“Hatua ya kuwarejesha wagombea wetu wote walioenguliwa bila sababu ni hatua muhimu, tunaitaka Tamisemi isimamie maelekezo yake kikamilifu kwa sababu tumeshuhudia wasimamizi wa uchaguzi wakidharau maelekezo ya kikanuni,” amesema.

Mbali na hilo, Ado ameitaka Serikali kuhakikisha haki inatendeka katika hatua muhimu zilizobaki za uchaguzi serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, ikiwemo kampeni, uapishaji mawakala, upigaji kura hadi kutangazwa washindi.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema hakuwa mbali na maelezo ya Ado akisisitiza Tamisemi kuchukua hatua kwa wale watakaobainika kuengua wagombea kinyume cha kanuni ili iwe fundisho na kurejesha amani.

Katika taarifa ya kwa umma, Mrema pia aliwaagiza wagombea wasiopata fursa ya kuwasilisha rufaa zao kufanya hivyo baada ya muda kuongezwa na Tamisemi.

“Tamisemi imeagiza fomu za wagombea walioenguliwa ziwasilishwe wilayani, wito wetu wagombea walioenguliwa kinyume cha utaratibu, warejeshwe kugombea ili tuwape nafasi wananchi kuchagua viongozi.”

Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kinondoni, Henry Kileo ametaka haki itendeke katika hatua ya kuwarejesha wagombea 72 walioengeuliwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukosa udhamini wa chama.

 Kileo amesema taarifa walizonazo wagombea wao huenda watarejeshwa lakini sio maeneo ambayo ndio ngome zao.

“Wamekata watu wetu, lakini watakwenda kuwarudisha wachache kwenye rufaa, lakini zile sehemu ambazo Chadema wana nguvu au ngome ya chama hawatawarudisha, isipokuwa watarudisha ile mitaa kwa sababu hivi ni vyama vya siasa kuna maeneo una nguvu na mengine huna nguvu.

“Hatutaki majina mengine yarudi na mengine yasirudi, maana sababu zao hazina mantiki wala tija fomu zilijazwa kwa uangalizi mzuri na ubora chini ya mawakili wa Chadema,” amesema Kileo.

Related Posts