Auwsa yafafanua upatikanaji wa maji Kijiji cha Oltepes

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (Auwsa) wilayani Longido imetoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa maji wilayani humo sambamba na miundombinu iliyopo zikiwamo mita za maji.

Ufafanuzi huo umekuja siku moja baada ya Novemba 12, 2024 Mwananchi kuripoti changamoto ya uhaba wa maji katika Kijiji cha Oltepes kilichopo Kata ya Orbomba wilayani humo iliyoeleza hali ya upatikanaji wa maji inavyowalazimu wasichana na wanawake wa eneo hilo kutumia siagi ya ng’ombe ili kudhibiti damu ya hedhi na mkojo wa ng’ombe kujisafisha.

Meneja wa Auwsa Wilaya ya Longido, Injinia Anord Kemkanju amesema wamefika kwenye boma ya mteja wao Elizabeth Olodo na kujiridhisha ni mteja hai, ana maji na miundombinu yote ipo na maji yanatoka saa 24.

“Miundombinu hii ya maji imeunganishwa moja kwa moja kwenye mradi mpya uliojengwa hapa Longido, ambapo sasa tenki letu kubwa linasambaza maji lipo mita 300 kutoka hapa tulipo. Hawa wameunganisha na bomba linalokwenda kwa DC (Mkuu wa Wilaya) na DAS (Katibu Tawala wa Wilaya).

“Kwahiyo maeneo haya yote yanapata maji kwa saa 24, hatujapata changamoto kwamba hakuna maji eneo hili,” amesema Injinia Kemkanju.

Hata hivyo, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido umesema kuwa Oktoba 16, 2024 halmashauri ilipokea wageni kutoka taasisi ya Baraza la Wanawake wa Kimaasai (PWC) pamoja na mwandishi wa habari kutoka gazeti la Mwananchi.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Mawasiliano Serikalini Wilaya ya Longido, Happiness Nselu imeeleza kuwa Shirika hilo na mwanahabari huyo walikuwa wakifuatilia suala la matumizi ya taulo za kike kwa wanafunzi wa shule za Sekondari zilizopo Wilayani Longido.

“Wakati wa ziara hiyo, walifanya mahojiano na mama Elizabeth Olodo (40), mkazi wa kijiji cha Longido, wilayani Longido, na sio mkazi wa kijiji cha Oltepesi kama ilivyoandikwa gazetini.

“Mama Elizabeth alieleza historia ya enzi za kale za jamii hiyo za matumizi ya vitambaa kabla ya ujio wa taulo za kike. Hata hivyo, upatikanaji wa taulo za kike kwenye shule za sekondari zilizopo Longido ni zaidi ya asilimia 98,” amesema.

Aidha, amesema shule za sekondari pia zimekuwa zikitenga bajeti ya wastani wa jumla ya Sh19 milioni kila mwaka, kwa ajili ya kununua taulo za kike kwa watoto wasiokuwa na uwezo wa kujinunulia.

“Vile vile, madai ya changamoto ya ukosefu wa maji katika vijiji vya Oltepesi na Longido yenyewe hayana msingi kwani, kwa sasa upatikanaji wa maji safi na salama ni zaidi ya asilimia 60 na Mamlaka maji bado inaendelea na jitihada za kuboresha zaidi huduma katika vijiji hivyo.”

Nselu amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya maji na inashirikiana bega kwa bega na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana kwa uhakika.

Novemba 12 gazeti la Mwananchi iliandika habari kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji katika kijiji cha Oltepes kilichopo Kata ya Orbomba, wilayani Longido inayowalazimu wasichana na wanawake wa eneo hilo kutumia siagi ya ng’ombe ili kudhibiti damu ya hedhi na mkojo wa ng’ombe kujisafisha.

Kuhusu tatizo la maji, Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido Dk Steven Kiruswa alithibitisha kuwa upatikanaji wa maji katika eneo hilo umeongezeka hadi asilimia 56, kutoka asilimia 36 miaka saba iliyopita.

Related Posts