Mazoea ya tabia ni mojawapo ya sababu iliyotajwa kuchangia ongezeko la ugonjwa Kichocho, au Kisonono cha damu katika Bonde la Ziwa Victoria. Jamii za eneo hili hasa wavuvi wakihusishwa na uchafuzi wa Ziwa kutokana na kufanya haja ndogo na kubwa ndani na ufuoni mwa Ziwa wanapokuwa katika shughuli za uvuvi, za kinyumbani na shughuli nyinginezo binafsi kama vile kufua, kuoga na biashara.
Mtafiti kutoka taasisi ya kitaifa ya utafiti na matibabu KEMRI Dkt. Maurice Odiere anasema majimbo yanayopakana na Ziwa Victoria ya Kisumu, Migori, Homabay, Siaya na Busia yanasajili maambukizi mengi ya ugonjwa wa kichocho, hatua ambayo imechochea mpango wa serikali kutoa dawa za kukabili ugonjwa huo katika maeneo hayo.
“Ziwa Victoria ndio chanzo kikuu cha maambukizi katika jamii na mazoea ya kwenda haja sehemu za wazi. Mfano wavuvi wanapoenda kuvua pengine usiku mzima, hili wanalifanya katika mikondo ya maji. Ndiyo sababu tunapendelea shinikizo la WHO kusisitiza kutolewa dawa kwa jamii kwa ujumla,” amesema Odiere.
Mpango wa serikali kupambana na ugonjwa wa kichocho mjini Kisumu
Chini ya mpango huu, serikali inatilia maanani kupambana na ugonjwa wa Kichocho kwa kuwekeza katika kuimarisha mifumo ya afya. Ikiwemo kutoa mafunzo kwa wahuhudumu wa afya mpango unaopigwa jeki na kampeini ya utowaji dawa kutokana na mchango wa shirika la afya duniani WHO.
Unaweza pia kusoma: Mripuko wa kipindupindu Kenya
Uhamasishaji na ushirikiano zaidi kati ya wadau wote katika ulingo wa afya, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, katika kiwango cha kitaifa na jimbo, ni hatua mojawapo inayohimizwa, kama malengo ya kudhibiti maambukizi.
Mwanaharakati wa mazingira Ziwa Victoria kutoka shirika la kimazingira la Ianna, Malaika Mary Atieno, anapendekeza kuwekwa vyoo zaidi vinavyozingatia mazingira salama maeneo ya ufuoni, kuwafaa zaidi wavuvi na wengine walio na shughuli katika sehemu za fuo.
“Tunajaribu kuwaelimishwa wavuvi na wale wanaofanya biashara Ziwa Victoria na wale wanaoishi kwanza kuhusu kutunza Ziwa. Kwanza kwa wavuvi wanapoenda kuvua samaki, unajua wanaenda usiku wa manane, na ukitoka hapa hadi kwenye wanaenda sio mahali pa kusema ni dakika 20 au 10 na warudi hapana, wanaweza toka kitu saa tatu warudi kitu saa kumi asubuhi, hayo masaa zote wako ndani ya maji mtu akitaka kuenda haja ndogo, haja kubwa hebu jiulize wanaenda wapi? Kujisaidia ni hapo hapo wakisonga,” amesema Atieno.
Magharibi mwa Kenya linakabiliwa na makali ya Kichocho
Kando na Nyanza, eneo jumla la Magharibi mwa Kenya linakabiliwa na makali ya Kichocho.
Unaweza pia kusoma: Mgomo wa madaktari waathiri hospitali za umma Kenya
Kulingana na utafiti wa mwaka 2022 ulioendeshwa na wizara ya afya na shirika la AMREF Africa ukibainisha, watu milioni 6 kutoka majimbo ya Vihiga, Bungoma, Kakamega na Tranza Nzoia wapo katika hatari ya kupata ugonjwa unaosababishwa na minyoo ya utumbo na kichocho.
Ugonjwa wa Kichocho unaosababishwa na kimelea cha mnyoo bapa, kwa lugha ya kitaalamu ‘Schistosoma’ ambao hupatikana zaidi katika mito na maziwa maeneo ya tropiki Afrika, Marekani ya Kusini na Asia, hupenyeza kwenye ngozi na kusafiri kupitia damu na kuvamia utumbo au kibofu cha mkojo. Dalili zake ni pamoja na muwasho, homa, udhaifu, maumivu ya tumbo na misuli kuuma.
Shirika la WHO limeuorodhesha ugonjwa wa kichocho miongoni mwa magonjwa 21 ya kitropiki yanayotazamiwa kukomeshwa kufikia mwaka 2030.