Alfajiri ya simanzi iliyomsababishia upofu

Dar es Salaam. Alfajiri ya Agosti 13, 2024 haiwezi kufutika kichwani mwa Esther Makaranga (25) kutokana na tukio lililobadili maisha yake.

Esther, mama wa watoto wawili siku hiyo ilikuwa mwisho wa kuona kutokana na kudai kutobolewa macho na mtu anayemtaja kuwa ni mume wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi anakiri kufahamu tukio hilo na anaeleza mtuhumiwa ni Paulo Shija (37), ambaye ni mume wa mama huyo na sasa kesi inashughukiliwa na mahakama.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi kijijini kwao Kundikiri, Esther anaeleza mwaka 2021 alikwenda Shinyanga mjini kujitafutia maisha akitokea Kijiji cha Kundikiri wilayani Kahama alikokuwa akiishi na wanawe na mama yake.

Akiwa mtoto wa tatu kati ya watoto saba kwenye familia yao, Esther anasema aliishia darasa la tatu akajikita kwenye kilimo ili kusaidiana na ndugu zake kuendesha familia na kumhudumia mama yao aliyeanza kuugua muda mfupi baada ya baba yao kufariki dunia.

Kutokana na ugumu wa maisha kijijini, alikwenda Kahama mjini alikofanya kazi za ndani kabla ya dada yake anayeishi Shinyanga kumtafutia kazi kwenye mashine.

Kutokana na kazi hiyo, alipanga chumba chake na kuanzisha biashara ndogondogo ya kuuza nyanya.

“Baadaye nikaona niache kazi ili nipate muda mwingi wa kufanya biashara, nikawa nachukua bidhaa sokoni nakuja kuuza nje ya nyumba nilipokuwa naishi,” anaeleza.

Akiwa katika biashara ndipo alipokutana na Shija aliyekuwa mlinzi kwenye nyumba ya kulala wageni, wakaanzisha uhusiano uliowaingiza kwenye ndoa Septemba 16, 2023.

Hata hivyo, baada ya kufunga ndoa anaeleza mambo yalibadilika kutokana na ugomvi, hivyo alirejea kwao kijijini alikoendelea na kilimo.

Anadai alipofikwa na kadhia hiyo alikuwa Shinyanga kufuata vitu vyake baada ya ndoa yao kuvunjika.

Akizungumza na Mwananchi Mwenyekiti wa Mtaa wa Banduka, Pius Shilinde anaeleza siku ya tukio alifuatwa na wananchi waliomweleza kuhusu uwepo wa mwanamke aliyejeruhiwa.

“Nilifika eneo la tukio sikuweza kumtambua huyo mwanamke, uso wake ulikuwa umevimba hivyo haikuwa rahisi kwangu kumtambua kama ni mkazi wa mtaa wangu au la, nilichofanya nikawasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga akawatuma askari wakaja.

“Wakati tukiendelea kusubiri askari wafike yule msichana akajieleza kwamba ana dada yake hapa, bahati nzuri akatokea mtu anayemfahamu huyo dada yake ila hakuwa anaishi mtaani kwangu alikuwa mtaa wa jirani tukamuagiza akamfuate na hilo likafanyika akaja eneo la tukio,” anasema.

Lucia Makaranga, dada wa Esther anasema alipata taarifa za kuwepo mtu aliyeshambuliwa anayejitambulisha kuwa ndugu yake lakini hakukubaliana nazo kwa sababu hakuwa akifahamu kama mdogo wake aliingia Shinyanga bila kumtaarifu.

“Nilichokuwa nafahamu Esther yupo nyumbani kijijini, sikuwa na taarifa za ujio wake mjini hivyo nilipoambiwa kuna ndugu yangu ameshambuliwa nilikataa, aliyenifuata akanisihi niende eneo la tukio. Hata hivyo sikumtambua alikuwa ameharibika hadi aliponiita kwa jina.

“Nilishtuka, tukampeleka hospitali, haikuwa rahisi kwa sababu hatukuwa na fedha watu wa ustawi wa jamii walitusaidia katika hatua za awali lakini baadaye wakatuacha kwenye Hospitali ya Kolandoto ambako ilionekana kuna wataalamu wa macho wangeweza kumsaidia,” anasema.

Anasema baada ya uchunguzi ikabainika macho ya Esther yameharibika anahitaji kufanyiwa upasuaji ambao gharama yake ni Sh460,000. Walizungumza na uongozi wa hospitali upasuaji ukafanyika ingawa hawakuwa na fedha.

“Baada ya kufanyiwa upasuaji ikaonekana jicho moja limeharibika kabisa hawezi kuona ila lingine linaweza kutibiwa.

“Daktari aliyekuwa akimhudumia akasema matibabu hayo yanaweza kufanyika KCMC na nilipofuatilia kujua inaweza kugharimu kiasi gani nikabaini si chini ya milioni moja, kwa kuwa sikuwa na uwezo huo tukaishia hapo nikiendelea kumuangalia mdogo wangu akipitia maumivu makali,” amasema.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kolandoto, Joseph Sahani anasema baada ya kumpokea Esther alifanyiwa vipimo walibaini macho yake yametobolewa na kitu chenye ncha kali na jicho la kushoto lilikuwa limeharibika kabisa hivyo wakalazimika kulitoa.

Anasema unafuu ulionekana kwenye jicho la kulia, wataalamu walifikiri angepata matibabu ya kina zaidi huenda lingeweza kupona na kuona.

 “Nafikiri hadi sasa hajaenda kwa sababu ya changamoto za kiuchumi ila ukweli ni kwamba kadiri anavyokaa muda mrefu bila kupata matibabu muhimu ikiwemo kuiondoa damu hiyo, uwezekano wa kulitibu unazidi kupungua.

“Kwa tatizo alilonalo ikizidi mwezi mmoja baada ya jicho kupata jereha, ufanisi wa matibabu unazidi kupungua hivyo tunamshauri aende akapate matibabu,” anasema.

Dk Sahani anawaomba watu watakaoguswa wamsaidie Esther ili akapatiwe matibabu.

Esther anaeleza hali aliyonayo inamuongezea umasikini kwenye familia kwa kuwa yeye ndiye alikuwa akitegemewa na watoto wake wawili na mama yake mzazi.

Anasema kupitia kilimo na biashara ndogondogo alimudu kupunguza makali ya maisha na alihakikisha watoto wake wanaenda shule lakini sasa haoni hilo likiendelea katika hali yake ya ulemavu wa macho.

“Kuna wakati namuuliza Mungu kwa nini nilizinduka siku ile ya tukio, labda angeniacha nipite kuliko hiki ninachopitia. Nimezoea kuishi nikiwa na macho yangu mawili nahangaika huku na kule kuhakikisha familia yangu inaenda lakini sasa nimekuwa mzigo, kutokana na hali yangu ya upofu siwezi kufanya chochote.

“Watoto waliokuwa wananitegemea sijui hatima ya maisha yao, mzazi mwenzangu alinitelekeza tangu wakiwa wadogo nimekuwa nikihangaika nao mwenyewe, nilikuwa najishughulisha na vibiashara vidogovidogo na kilimo naweza kuwahudumia lakini sasa siwezi tena,” anasema.

Pia, hawezi kufanya kwa ufanisi shughuli zinazohusu mahitaji yake ya kimwili na huenda suala hilo likamuathiri kisaikolojia.

Lucia anaeleza mdogo wake kwa sasa hawezi kukaa mwenyewe, hivyo inamlazimu hata yeye kuacha shughuli zake za utafutaji ili kumuangalia wakati wote.

“Angalau amejifunza njia, chooni anaweza kwenda lakini ni lazima umpelekee maji na wakati mwingine anahitaji msaada. Hali yake ndiyo hivyo kama unavyomuona kila kitu ni lazima umsogezee hivyo hakuna namna unaweza kumuacha peke yake.

“Ukiondoa usaidizi wa aina hiyo amekuwa na woga uliopitiliza, akikaa peke yake anakuwa na wasiwasi anaogopa hata akisikia hodi hivyo ni lazima muda wote niwe naye. Anapitia hali ngumu, niwaombe Watanzania waguswe na hali yake wamsaidie apate matibabu ya jicho moja ambalo tumeambiwa angalau linaweza kuona,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro anasema Serikali ilichukua hatua kuhakikisha anapata matibabu katika Hospitali ya Kolandoto na baada ya hapo mpango ulikuwa apewe rufaa kwenda Bugando lakini madaktari wakashauri vingine.

“Baada ya madaktari kufanya uchambuzi wa kina ikaonekana hospitali ambayo inaweza kufanya matibabu na kumrejeshea uoni wake angalau kwa jicho moja ni KCMC, kwa hiyo upande wa Serikali tulikubaliana kwamba mwezi huu wa Novemba tuanze kukamilisha utaratibu wa vibali vya msamaha ili aweze kusafiri kwenda kupata matibabu.

“Ufuatiliaji wa awali pale KCMC umeonyesha matibabu ambayo yatawezesha kurejesha hilo jicho moja yanagharimu zaidi ya Sh12 milioni, tunafahamu kwa hali yake hawezi ndiyo maana Serikali tumelichukua na kuanza taratibu za matibabu ya msamaha ili kuzibeba gharama zote hizi,” anasema.

Mtatiro anatoa wito kwa wakazi wa Shinyanga kutoa taarifa mapema zinapotokea dalili au viashiria vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na siyo kusubiri hadi ukatili huo ufanyike.

“Kwa uzoefu wa matukio haya huwa yana viashiria, hayaibuki ghafla na kutendeka. Wanaofanya matukio ya aina hii ni watu tunaoishi nao, niwaombe wananchi wanapoona dalili za matukio ya aina hii watoe taarifa kwa mamlaka husika.

Imeandaliwa kwa kushirikiana na Bill and Melinda Gates Foundation

Related Posts