VIDEO: Polisi yaanza uchunguzi mauaji ya Katibu wa CCM Kilolo

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linachunguza tukio la mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, Christina Nindi (56).

Nindi ameshambuliwa kwa kupigwa risasi kifuani pamoja na kitu kizito na watu wasiojulikana.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 13 na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Allan Bukumbi amesema Nindi ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Banawani, Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke na Tarafa ya Mlolo, ameshambuliwa usiku wa kuamkia leo.

“Bunduki iliyotumika kumpiga risasi tunadhani ni aina ya Shotgun baada ya askari kuokota maganda na gorori ndogo eneo la tukio,  lakini pia tulipomkagua, tumebaini alipigwa pia na kitu kizito kichwani na uchunguzi wa awali unaonyesha ameshambuliwa na vijana watatu ambao walitokomea kusikojulikana,” amesema kamanda huyo.


Polisi waanza uchunguzi mauaji ya Katibu wa CCM Kilolo

Amesema uchunguzi wa awali, unaonyesha Nindi alivamiwa na vijana watatu wasiojulikana nyumbani kwake  anakoishi na binti zake wawili.

“Watu hao wasiojulikana walimshambulia binti mmoja wa marehemu na kumjeruhi usoni, pamoja na jirani yake ambaye alipigwa na kitu butu upande wa ubavu wa kushoto alipokuwa akijaribu kutoa msaada baada ya kusikia kelele kutoka kwa binti wa marehemu,” amesema  kamanda huyo.

Aidha, amesema baada ya shambulio hilo, washambuliaji hao walitoroka bila kuchukua kitu chochote.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na jitihada zinafanyika kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Viongozi wa CCM Mkoa wa Iringa wakiwa nyumbani kwa marehemu, Christina Kibiki katika Kijiji cha Ugwachanya (wa kwanza kushoto ) Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM (NEC) Mkoa wa Iringa, Salim Abri Asasi akiwa na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Daudi Yasin (kulia) wakijadili jambo. Picha na Mary Sanyiwa.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kuwakamata wahalifu hao kuzifikisha kwa mamlaka husika ili ziweze kufanyiwa kazi.

Awali, akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassini amelaani mauaji hayo huku akieleza alikuwa miongoni mwa watendaji waaminifu na wachapakazi wa muda mrefu ndani ya chama chao.

“Tukio hili la kikatili limeondoa uhai wa katibu wetu wa Wilaya ya Kilolo. Tumepokea taarifa hizi kwa masikitiko makubwa, hasa ukizingatia kuwa Katibu Nindi alikuwa akifanya kazi kwa moyo na kujituma kwa ajili ya kukipigania chama,” amesema Yassini.

Aidha, Yassini ameongeza kuwa tukio hilo limetokea wakati chama kikiwa katika maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na katibu ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za chama.

Mmoja wa watoto wa marehemu Christina Kibiki, ambaye alishuhudia tukio hilo akizungumza na waandishi wa habari akiwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Ugwachanya.

Ameomba wafiwa na wanachama wa CCM kuwa watulivu katika kipindi hiki cha maombolezo, huku akisisitiza kuwa, vyombo vya dola vinaendelea na juhudi za kuwasaka wahusika ili sheria ichukue mkondo wake.

Mwenyekiti huyo pia ametangaza kuwa maziko ya Nindi yanatarajiwa kufanyika Ijumaa Novemba 15, katika Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke, Tarafa ya Mlolo mkoani Iringa.

Mmoja wa watoto wa marehemu, ambaye alishuhudia tukio hilo, amesema watu watatu waliingia ndani na kuanza kumshambulia mama yake.

“Niliposikia mlio kama wa bunduki nilikimbilia nje kuomba msaada kwa majirani,” amesema mtoto huyo ambaye hata hivyo alishindwa kuendelea kusimulia.

Related Posts