Na Humphrey Shao, Michuzi Tv
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es salaam, Edward Mpogolo, ametoa wito kwa vijana kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na kuchagua viongozi wenye sifa, hekima, busara na ustamilivu.
Mpogolo ametoa wito huo katika kata ya Kitunda kwenye kongamano la burasa na hekima ya kijana kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa novemba 27 mwaka huu.
Akizungumza na kundi la vijana, viongozi wa dini ya kiislam kwa ngazi ya Mkoa, wilaya, kata na wageni mbalimbali, Mpogolo ameeleza umuhimu wa kushiriki uchaguzi huo kwa kuchagua viongozi wenye nia ya kuendeleza maendeleo.
Amesema uchaguzi wa serikali za mitaa, ni muhimu kuliko baadhi ya wananchi wanavyodhani kuwa hakuna haja ya kushiriki bali amebainisha nguvu ya uongozi wa mitaa kutokana na serikali kuu kushusha sehemu ya mamlaka kwa ngazi ya chini ili kurahisisha maendeleo ya wananchi.
Kupitia serikali za mitaa zipo fursa na uhitaji wa wananchi unaoanzia katika ngazi ya mtaa akitolea mfano barua za udhamini, na utambuzi ambazo zinahitajika na kupatikana kwa uongozi wa serikali za mitaa.
Akizungumzia kuhusu elimu ya ushiriki katika uchaguzi wa serikali za Mtaa, Mpogolo amesema halmashauri ya jiji imetoa elimu kwa kata 36 na mitaa 159 ili wananchi na makundi mengine yashiriki kujiandikisha na kujitokeza kupiga kura.
Katika kongamano hilo lililoandaliwa na Jumuia ya vijana wa Kiislam Bakwata ( JUVIKIBA), Mpogolo ametumia nafasi hiyo kuelezea kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa na Mh Rais Samia Suluhu Hassan katika miradi mbalimbali sekta ya Barabara, Elimu, Maji, na uchumi jui ya mikopo ya halmashauri ya jiji la ilala.
Aidha, zaidi ya shilingi bilioni 36 zimepokewa Ilala kwa ajili ya mradi wa maji tank linalojengwa Pugu Bangulo ambalo litamaliza na kuounguza kero ya maji kwa wananchi wa ukanda huo.
Akizungumzia sekta ya elimu ya msingi imepokea kiasi cha shilingi bilioni 28 wakati sekondari imepokea bilioni 18, na ushuhuda upo katika shule za kata zinazojengwa majengo ya ghorofa yenye uwezo wa kupokea wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.
Kuhusu mikopo ya halmashauri Mpogolo ameendelea kutoa hamasa kwa wananchi hasa makundi ya wanawake, vijana na walemavu watumie fursa ya elimu kuweza kukopa mkopo huo ambao Ilala ina zaidi ya bilioni 14 kuwawezesha wajasiriamali ili wakope na kurudisha.
Kwa upande wake Shekhe wa Mkoa wa Dar es salaam, Walid Alhadi amewataka waumini wa kiislam kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi serikali za mitaa na kuwapuuza watu wanaosema dini ya kiislam ni haramu kupiga kura.
Aidha, Shekhe Alhadi amempongeza Mkuu wa wilaya ya Ilala kwa kuwa karibu na matukio ya kijamii katika uongozi wake hali inayosaidia kujua taarifa mbalimbali za maendeleo.
Nao vijana waandaaji wa kongamano hilo wamesema wako tayari kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa na kuchagua viongozi bora baada ya kujua umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na kwa nini washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.