Kibaha/Njombe. Watu 12 kati ya 22 waliokamatwa kwa makosa ya rushwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Pwani wamehukumiwa baada ya kupatikana na hatia.
Kesi hizo zilifunguliwa katika mahakama za wilaya za Mkoa wa Pwani kati ya Julai na Septemba 2024, baada ya uchunguzi kubaini ukiukwaji wa sheria uliofanywa na wahusika.
Hayo yamesemwa leo, Jumatano, Novemba 13, 2024, na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani, Alli Sadiki alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.
Amesema kati ya kesi za rushwa zilizoshughulikiwa, 12 zimeshatolewa hukumu huku nyingine zikiendelea kusikilizwa.
Sadiki amesema baadhi ya waliohukumiwa walilipa faini na wengine walifungwa, wakiwamo watumishi wa umma na watu kutoka taasisi binafsi.
Katika hatua nyingine, Sadiki amesema Takukuru imesaidia kukusanya Sh1.5 bilioni kutoka kwa waajiri 77 waliobainika kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Waajiri hao walielimishwa na kupewa maelekezo ya kisheria na kufikia Septemba mwaka huu, walikuwa wamewasilisha michango hiyo.
“Baadhi ya waajiri hawakuwa wakijua kuwa kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwenye NSSF ni kosa kisheria, lakini baada ya kupewa elimu, walikubali kutekeleza agizo hilo,” amesema Sadiki.
Akizungumzia tatizo la waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati, Amina Nassoro, mkazi wa Kibaha, amesema linawaathiri wafanyakazi wengi wa sekta binafsi. Akitoa mfano wa wafanyakazi wa viwandani, amesema baadhi ya waajiri wanawakata mishahara lakini hawapeleki michango hiyo NSSF, hali inayowaathiri wanapofikia umri wa kustaafu kwa kuwa hukosa mafao au hupata kwa kuchelewa sana.
“Hii ni changamoto kubwa na Serikali inapaswa kuzingatia masilahi ya wananchi wake ili kuepuka kuwachelewesha kimaendeleo,” amesema Nassoro.
Wakati huo huo, Takukuru Mkoa wa Njombe imewataka wananchi kutoa taarifa mara wanapogundua viashiria vya rushwa katika maeneo yao, hasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024. Naibu Kamanda wa Takukuru Njombe, Noel Mseo amesema kuwa wamejipanga kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi kwa kushirikiana na wananchi, vyama vya siasa na wadau mbalimbali.
Ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya rushwa ili hatua zichukuliwe mapema.
Aidha, amesema Takukuru Njombe inaendelea kufuatilia mienendo ya wagombea na vyama vya siasa ili kubaini kama kuna viashiria vya rushwa na kuchukua hatua kwa watakaobainika.
“Kama itadhihirika na kuna ushahidi wa wazi kuwa kuna mtu ametenda kosa kwa kukiuka sheria, tutachukua hatua kwa kuanza uchunguzi na hatimaye kulifikisha shauri mahakamani,” amesema Mseo.
Amesema katika kipindi cha miezi mitatu, Takukuru Mkoa wa Njombe imefuatilia na kukagua miradi 33 katika sekta ya elimu, afya, barabara, mifugo, maji na ujenzi wa nyumba za watumishi yenye thamani ya Sh5.4 bilioni. “Miradi mitano yenye thamani ya Sh579.3 milioni ilibainika kuwa na upungufu na hatua mbalimbali zimechukuliwa kurekebisha upungufu huo,” amesema Mseo.