UJENZI WA MADARAJA YA MAWE CHINI YA TARURA WAOKOA BIL. 52

Takribani Bil. 52 zimeokolewa na serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA katika ujenzi wa madaraja ya mawe zaidi ya 335 ambapo ni teknolojia iliyoanzishwa na shirika la ENABEL la nchini Ubelgiji kwa kushirikiana na TARURA.

Hilo limebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe.Mohamed Mchengerwa katika ziara ya kukagua miradi iliyotekelezwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Ubelgiji kupitia shirika la ENABEL katika mkoa wa Kigoma.

Mhe. Katimba amesema “shirika hili la ENABEL limeshiriki kwa kiwango kikubwa sana katika utengenezaji wa madaraja kwa njia ya mawe na mpaka muda huu kwa kutumia hii Teknolojia ambayo ENABEL waliibuni kwa kushirikiana na TARURA mpaka sasa kuna madaraja zaidi ya 335 ambayo yamejengwa kwa teknolijia ya mawe
Tanzania nzima” Amesema

Akizungumza umuhimu wa Teknoloji hiyo Mhe. Katimba ameongeza kuwa “Daraja
ambalo limetengenezwa kwa njia ya mawe linakaa kwa miaka 200 na kuendelea lakini pia kwa haya madaraja 335 ambayo sisi TARURA tumejenga Tanzania nzima tumetumia shilingi Bilioni 19 lakini kama tugetumia teknolojia ya kawaida tungetakiwa kuwa na Bilioni 71″ amesema.

Miradi iliyotembelewa ambayo Tanzania imeshirikiana na Ubelgiji kupitia shirika la ENABEL ni daraja la Mawe la Bweru,mradi wa Maji Mwayaya wiłaya ya Buhigwe,mradi wa WEZESHA BINTI na Kituo cha Walimu wilaya ya Kasulu.

Ugeni huo kutoka nchini Ubelgiji upo mkoani Kigoma ukiongozwa na Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Mhe. Peter Huyghebaert akiwa ameambatana na mkurugenzi mkuu wa shirika la ENABEL Bw. Jean Van Wetter pamoja na viongozi mbalimbali kwaajili ya kusherehekea miaka 25 ya uwepo wa shirika hilo nchini Tanzania pamoja na miaka 40 ya ushirikiano wa Tanzania na Ubelgiji.

Related Posts