Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema, Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) linalojengwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga ujenzi wake umefikia asilimia 47.1.
Akizungumzia ujenzi wa bomba hilo, leo Jumatano, Novemba 13, 2024, Mratibu wa mradi huo, Siadi Mrutu amesema katika utekelezaji wa mradi huo tayari watu 9,858 wamelipwa fidia kati ya 9,927 wenye madai ya kulipwa fidia na hadi sasa wenye madai ni 69 pekee.
“Mradi uliwaahidi kuwajengea nyumba wakazi 294 hadi sasa nyumba 340 zimekamilika na tayari wananchi hao washakabidhiwa na kuhamia kwenye nyumba zao, shughuli hii ilikwenda sambamba na uhamishaji makaburi 1,146,” amesema.
Amesema mradi wa EACOP umezalisha ajira 8,694 kwa Watanzania tangu kuanza kwa mradi Februari 2022 na fursa hizo za ajira zitaendelea kutoka kadri makandarasi watakavyoingia.
“Utaratibu wa hizi ajira hakuna kutoa fedha ili upate kazi, hakuna kutoa rushwa kwani zoezi linashirikisha Serikali za mitaa ili kuweza kufanya usahili hasa kwa ajili ya nafasi ambazo hazina utaalamu,” amesema Mrutu.
“Mradi umeboresha bomba la maji kwenda mji wa Muheza na kulibadili kutoka kwenye ukubwa wa kipenyo cha inchi sita mpaka inchi nane lenye uwezo wa kusafilisha maji lita milioni 2 kwa siku, hivyo kuboresha huduma ya maji kwenye Mji wa Muheza,” amesema mratibu wa mradi.
Sambamba na hayo, Serikali imepata mapato yenye jumla Sh50 bilioni kupitia vibali, pango la ardhi ya mradi, tozo za halmashauri, huduma za umeme, maji, uondoshaji maji taka, ulinzi na kodi za kampuni zinayohudumia mradi.
Hadi sasa utekelezaji wa mradi unahusisha, ujenzi wa kambi 16 za kutunza vifaa na makazi ya wafanyakazi na kambi nne zipo Uganda na kambi 12 zipo Tanzania.