UJIO wa Valentin Nouma ndani ya kikosi cha Simba ulikuwa na matumaini makubwa kwa mashabiki na viongozi wa timu hiyo, wakiamini ataongeza nguvu eneo la ulinzi, lakini hadi sasa kwenye mechi kumi za ligi zilizochezwa na Simba ametumika kwa dakika 185 katika mechi nne.
Beki huyo wa kushoto alisajiliwa na Simba kwa ajili ya kusaidiana na nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye ameitumikia Simba kwa misimu 11 sasa tangu alipojiunga nayo mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.
Januari 2025, Tshabalala atakuwa amebakiza miezi sita ya kuitumikia timu hiyo na ni wazi kwamba Simba watakuwa na kazi kubwa kuhakikisha wanambakisha kutokana na ofa kibao ambazo ameanza kuzipokea.
Msimu uliopita mchezaji huyo alihusishwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na msimu huu pia kuna ofa kadhaa zinatajwa, Simba ikiwa bado inaendelea kuhitaji huduma yake kutokana na kushindwa kupata mbadala wake sahihi.
Dirisha kubwa la usajili lililopita Simba walimshusha Nouma raia wa Burkina Faso ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo akitokea FC Saint Eloi ya DR Congo.
Tangu ametua Simba dirisha kubwa la usajili msimu huu, ni mara moja pekee Nouma amefanikiwa kucheza mechi ya kimashindano kwa dakika zote tisini, ilikuwa mechi ya ligi dhidi ya KMC wakati Simba iliposhinda 4-0.
Beki huyo mchezo wake wa kwanza wa ligi kucheza alitokea benchi dhidi ya Dodoma Jiji akichukua nafasi ya kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua ambapo alitumika kwa dakika 11 Simba iliposhinda bao 1-0 ugenini.
Mchezo wa pili kwake ulikuwa ni dhidi ya Namungo FC aliocheza kwa dakika 74, Simba ilishinda 3-0, kisha dhidi ya Mashujaa (dk 10).
Licha ya kupata dakika chache na timu yake kuibuka na ushindi katika mechi zote nne alizocheza, hajahusika kwenye mchango wowote wa bao kwani hajafunga wala kuasisti kulinganisha na Tshabalala ambaye ametumika zaidi yake kwa dakika 697 kwenye mechi tisa akikosa moja pekee ya ligi.
Tshabalala yupo Simba tangu 2014 alipojiunga na timu hiyo akitokea Kagera Sugar na hadi sasa amekutana na mabeki kutoka mataifa mbalimbali katika kikosi hicho, wakiwemo pia wale wa ndani lakini amefanikiwa kuwazidi uwezo.
Alianza Jamal Mwambeleko ambaye licha ya kiwango bora alichokuwa nacho wakati huo akiwa Mbao, lakini ujio wake ndani ya Simba ilikuwa changamoto kwake kwani alishindwa kupenya mbele ya Tshabalala na baadaye aliomba kuondoka kutokana na kukosa nafasi.
Mwingine ni Mghana, Asante Kwasi ambaye alionekana huenda akapindua meza na kuondoa ufalme wa Tshabalala aliposajiliwa msimu wa 2016/17 akitokea Lipuli ya Iringa. Licha ya kuwa na uwezo mzuri wa kuzuia na kushambulia, lakini hakutoboa.
Kwa kiasi fulani alifanikiwa kumuweka benchi, lakini hakuchukua muda wa kujidai zaidi na mwisho alikubali kushindwa akaondoka ndani ya kikosi hicho msimu wa 2018/19 na kutua Hafia ya Guinea.
Maisha ndani ya kikosi cha Simba yaliendelea vizuri kwa Tshabalala akiendelea kucheza kikosi cha kwanza hadi Simba walipomletea Gadiel Michael akijiunga na kikosi hicho 2019 akitokea Yanga ambapo alikuwa anacheza kikosi cha kwanza, lakini mbele ya Tshabalala mambo yalikuwa magumu, benchi likawa ndiyo maskani kwake.
Hao ni baadhi tu ya mabeki walioushindwa muziki wa Tshabalala ndani ya Simba na kuamua kwenda kutafuta changamoto kwenye timu nyingine ili kulinda vipaji vyao.
Swali ni je? Nouma ataweza kupindua meza mbele ya Tshabalala licha ya kuchelewa kuanza vyema msimu wake wa kwanza akimpisha beki huyo kuendeleza makali yake?