Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imejipanga kutumia teknolojia ya kidijitali kuleta mapinduzi katika utoaji wa huduma za afya kwa kuunda mfumo wa afya unaowezeshwa kidijitali ambao ni bora, wenye usawa na unaozingatia huduma kwa mgonjwa, imeelezwa.
Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui ameeleza hayo leo Novemba 13, 2024 alipofungua mafunzo ya awamu ya pili ya afya ya kidijitali Zanzibar yenye lengo la kujadili na kuchunguza uwezekano wa mabadiliko ya afya ya kidijitali katika kuimarisha afya na ustawi wa jamii.
“Mpango huu utawawezesha wafanyakazi wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) kutoa huduma muhimu za afya kwa kuwapa vifaa vya kidijitali vitakavyoimarisha shughuli zao, ikiwamo ukusanyaji wa takwimu zitakazosaidia kuonyesha uhalisia wa maradhi yaliyopo kwenye jamii na milipuko inayotokea,” amesema.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na wananchi washirika wa maendeleo na sekta binafsi, watahakikisha wanadumisha mpango huo ili kufikia vipaumbele vya afya vya kitaifa.
Amezitaka taasisi na mashirika ya maendeleo kuimarisha ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kufikia malengo ya mkakati wa afya wa kidijitali wa 2020-2025.
Amesema taaluma itakayotolewa kwa wafanyakazi hao ni sehemu ya kufikia malengo ya Serikali ya kuhakikisha mifumo ya takwimu na taarifa inakuwa ya kidijitali kwa lengo la kufanya maamuzi sahihi katika kufikia huduma za afya kwa wote na afya bora.
Ameishukuru taasisi ya D-tree kwa ushirikiano katika mipango ya afya ya jamii na uwekezaji wa afya ya kidijitali ambao umesaidia kuongeza ufanisi kwa wahudumu wa afya ya jamii na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, Dk Mzee Suleiman Mndewa amesema miundombinu ya mawasiliano imeimarika, hivyo kuja kwa programu hiyo kutaendana na kasi ya mawasiliano iliyopo na kuwasaidia kufikia malengo.
Amesema ni wakati wa wahudumu kuongeza ubunifu kuhakikisha wanazalisha vitu vingi vitakavyoongeza tija kwenye sekta ya afya.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya, Dk Salim Slim amewataka kufanya kazi ipasavyo kwa lengo la kupunguza matatizo yaliyopo kwenye jamii yakiwamo ya kisukari, shinikizo la damu na maradhi yasiyoambukiza.
Mkurugenzi wa D-Tree Zanzibar, Dk Hannah Mikidadi amesema kwa muda mrefu wahudumu hao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali katika utendaji wao, hivyo mafunzo na vitendea kazi vya kidijitali viyawasaidia kuifikia jamii kwa haraka na kukusanya taarifa sahihi.
Msimamizi wa wahudumu wa afya ya jamii, Halima Ali Khamis amesema kuzinduliwa kwa mfumo huo kutawasaidia kupunguza gharama za matibabu, kutoa taarifa sahihi za takwimu zinazoongeza uwajibikaji kwa CHW na kufanya uchunguzi kwa baadhi ya maradhi kwenye jamii.