Dodoma. Wakati Bunge la Tanzania likipitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, Serikali imesema mwishoni mwa mwaka 2024 ndege kubwa ya abiria ya Boeing 737-9 Max itaanza kwenda Dodoma mara mbili kwa siku.
Pia, Serikali imesema wananchi wa Kipunguni jijini Dar es Salaam waliopisha uwanja wa ndege, wataanza kulipwa fedha zao mwaka huu, baada ya kusubiri kwa takriban miaka 27.
Hayo yamesemwa jana Jumatatu Mei 6, 2024 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge bungeni.
“Kuna hoja ya wabunge wa Kigoma, Rukwa na Katavi, nakubaliana na wabunge hawa kwamba wananchi wa mikoa hiyo wanapata shida ya usafiri wa majini,” amesema.
Profesa Mbarawa amesema Serikali kwa mwaka huu wa fedha imetengea jumla ya Sh10 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa meli mbili za MV Liemba na MV Mwongozo zote za Ziwa Tanganyika.
Amesema Sh5 bilioni ni kwa ajili ya ukarabati wa MV Liemba na Sh5 bilioni kwa ajili ya MV Mwongozo na kwamba huo mpango wa muda mfupi katika kuwezesha wananchi wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa wanaotumia usafiri wa maji ndani ya Ziwa Tanganyika kupata usafiri.
Pia, imesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wa maeneo mbalimbali nchini ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya ndege, likiwamo Jimbo la Segerea (Dar es Salaam) ambako kumetengwa Sh129 bilioni kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi hao.
Profesa Mbarawa alikuwa akijibu hoja za wabunge wakiwamo mbunge wa Segerea (CCM) jijini Dar es Salaam, Bonnah Kamoli aliyesema malipo ya fidia kwa wakazi wa Kipunguni waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege hayajalipwa na Serikali kwa takriban miaka 27 huku, wakazi wake wakiishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Pia, Profesa Mbarawa amejibu hoja ya mbunge wa Nkasi (Chadema), Aidan Kenan aliyelalamikia kukosekana usafiri Ziwa Tanganyika akisema ni miaka minane sasa wizara hiyo imekuwa ikiwataja kwenye vitabu lakini hakuna utekelezaji.
Kenan alisema kukosekana kwa meli ya mizigo kunaikosesha Serikali mapato kwa kuwa asilimia 60 ya mizigo kutoka Tanzania inakwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Boeing 737-9 Max kutua Dodoma
Profesa Mbarawa amesema kati ya Oktoba na Novemba Serikali itaanza kupeleka ndege kubwa ya abiria ya Boeing 737-9 Max kwa kuwa wasafiri ni wengi na ndege iliyopo haiwezi kutimiza mahitaji ya wasafiri wa Dodoma.
“Uwanja wetu sasa hivi hauwezi kuruhusu kutua ndege kubwa ya Max. Kati ya Oktoba na Novemba Uwanja wa Ndege wa Msalato utakuwa tayari na tutaanza kufanya kazi hiyo.
“Ingawaje jengo la abiria litakuwa halijakamilika mnara wa kuongezea ndege utakuwa haujakamilika, lakini ndege hiyo itaweza kutua kwa sababu tutajenga mnara wa muda wa kuongozea ndege pale, wakati umefika kuleta ndege kubwa Dodoma.
“Kwa siku moja hapa (Dodoma) tunaleta ndege nne, ndege hazitoshi, lakini tukileta ndege mbili kubwa zitaweza kukidhi mahitaji ya Dodoma. Pia, tutaleta ndege nyingine itaanzia Dar es Salaam kupitia Dodoma hadi Mwanza,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesema pia kuhusu ndege ya Air-Tanzania kwenda Pemba atahakikisha inakwenda kwa kuwa na yeye anatoka Pemba.”
Boeing 737 Max 9 ambayo toleo lake la kwanza lilitoka mwaka 2017 inatumia injini ya LEAP-1B inayotengenezwa na CFM International ya Marekani.
Gharama yake inatajwa kuwa Dola 128.9 milioni hadi Dola 135 milioni za Marekani (Sh323.79 bilioni hadi Sh339.12 bilioni).
Urefu wake ni mita 42.16 na upana wa mabawa yake ni mita 35.9 na inaendeshwa na marubani wawili na wahudumu wa ndani ya ndege wanne.
Tanzania imekuwa nchi ya nne barani Afrika kumiliki ndege hiyo baada ya Nigeria (18), Ethiopia (17) na Afrika Kusini (5).
Jumla ya oda za Max 9 tangu mwaka 2017 ni 5,651 hadi Agosti 31, 2023 zilizokwisha kufikishwa kwa wanunuzi ni 1,298.
Kwa mwaka huu tayari wamewafikishia wateja wao ndege 344 nyingi zikiwa ni Max 9.
Tofauti kubwa ya Max 9 na A220, ni uwezo wa abiria kwa kuwa A220 uwezo wake wa juu ni kupakia abiria 160 wakati Max 9 uwezo wake wa juu ni abiria 220.
Umbali wa kuruka bila kusimama Max ni kilometa 6,570 huku A220 ni kilometa 6,112 na uwezo wa kupaa ukiwa na mzigo ni tani 67.5 kwa A220 na tani 88.3 kwa Max 9.
Spidi ni kilometa 840 kwa saa A220 huku ya Max 9 ikiwa pungufu kwa kilometa moja kwa saa (839). Bei ya A220-300 inatajwa kuwa Dola 91.5 milioni za Marekani (Sh229.84 bilioni).