Mpanzu apewa Waarabu Dar, Fadlu afunguka

DESEMBA 15 mwaka huu ni siku inayosubiriwa kwa hamu kubwa sana na mashabiki wa Simba, kwani wanaweza kumshuhudia nyota wao mpya, Elie Mpanzu akianza kuitumikia rasmi timu hiyo baada ya kufunguliwa kwa usajili wa dirisha dogo.

Mpanzu ambaye alitambulishwa Simba Septemba mwaka huu, hajaanza kuichezea timu hiyo kutokana na kutua baada ya kufungwa kwa usajili wa dirisha kubwa.

Baada ya kukaa kwa muda bila ya kucheza mechi yoyote ya kimashindano, Desemba 15 mwaka huu Simba itakapokuwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, Mpanzu anaweza kuonekana uwanjani endapo Kocha Fadlu Davids atampa nafasi.

Hiyo inatokana na jinsi siku ya mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ndiyo usajili wa dirisha dogo utakuwa umefunguliwa huku winga huyo raia wa DR Congo akiwa na kibali cha kuanza kutumika.

Simba iliyopangwa Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika, itaanza kampeni yake hiyo bila ya Mpanzu atakayezikosa mechi mbili za kwanza dhidi ya FC Bravo Do Maquis ya Angola itakayochezwa Novemba 28, nyumbani na CS Constantine ya Algeria, Desemba 8 ugenini.

Winga huyo ambaye anatarajiwa kuanza na Waarabu Desemba 15, kwa upande wa michuano ya ndani anaweza kuibukia katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KenGold Desemba 18 mwaka huu wakiwa nyumbani.

Wakati Mpanzu akisubiri muda ufike, wapo mastaa wanaoendelea kukiwasha eneo la winga ndani ya kikosi hicho ambao ni Edwin Balua, Kibu Denis, Ladack Chasambi na Joshua Mutale.

Rekodi za mawinga hao bado haziridhishi kwani mpaka sasa Simba imecheza mechi 10 za ligi, huku Kibu akiwa amecheza tisa kwa dakika 552 bila ya kufunga bao wala kutoa asisti.

Kwa upande wa Mutale aliyecheza mechi saba kwa dakika 356, naye hajafunga wala kutoa asisti wakati Balua akifunga mabao mawili akitumika kwa dakika 317 akicheza mechi nane, huku Chasambi aliyecheza mechi nne kwa dakika 260 hajafunga wala kutoa asisti.

Kuhusu Mpanzu kuanza kuitumikia Simba, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Ukimtazama Mpanzu utaona tumekusudia kutengeneza timu ya aina gani, hasa vijana na kama anaongezeka basi anakwenda kuongeza moto zaidi.

“Sina majibu ya moja kwa moja lini hasa atatumika lakini alishakuwa kwenye mazoezi na wachezaji wenzake kwa muda mrefu, hivyo viongozi ndio watatoa taarifa ya mashindano gani ataanza kucheza.”

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa kikosi hicho, Fadlu David alisema mara baada ya kiungo huyo kuanza kazi ndani ya kikosi chake, anaamini nguvu kubwa itaongezeka hasa eneo la safu ya ushambuliaji, jambo ambalo linaongeza uwezekano wa kupata ushindi.

Alisema jambo linalomuumiza kwa sasa ni kumwona Mpanzu haingii uwanjani wakati anaona shauku ya kucheza aliyonayo, kwani muda wote amekuwa naye mazoezini tangu aliposajiliwa, ila hakuna namna kwani ndiyo kanuni zilivyo.

“Mpanzu ni winga anayejua kufunga na kutengeneza nafasi na licha ya kutokuwa tayari kucheza kutokana na taratibu, lakini mchezaji mwenyewe anajituma kwa nguvu mithili ya mtu anayeweza kucheza mechi ijayo.

“Nimegundua vitu vingi kwake na ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa kwani, anajua kufunga na kutengeneza nafasi, hivyo anatoa matumaini makubwa katika kikosi kuwa kuna kitu kikubwa atakwenda kukiongeza endapo ataanza kucheza na muda sio mrefu mashabiki watamuona.”

Beki wa kulia wa timu hiyo, Kelvin Kijili, naye amemzungumzia winga huyo akibainisha: “Mpanzu ni mchezaji mwenye balaa, nimemuona mazoezini na anatupa matumaini zaidi kwani kikosi kizuri ni kile chenye wachezaji wenye uwezo mzuri na kupata matokeo mazuri katika mechi.”

Related Posts