Kenya. Serikali ya Kenya imesisitiza shule zisifunguliwe kutokana na hali ya mafuriko inayoikumba nchi hiyo tangu mvua kubwa za El-Nino zilizoanza Machi mwaka huu.
Hayo yamebainishwa jana Jumatatu Mei 6, 2024 na Msemaji wa Serikali, Isaac Mwaura, wakati akizungumza kwenye kipindi cha Hot 96 Breakfast, amesema wakuu wa shule wazingatie agizo lililotolewa na Rais William Ruto.
Rais Ruto aliagiza Wizara ya Elimu kuahirisha kufunguliwa tena kwa shule zote hadi itakapotangazwa, akibainisha kuwa hali hiyo ya mafuriko huenda ikaongezeka siku zijazo.
Tovuti ya Citizen Digital imesema awali shule zilipangwa kufunguliwa Aprili 29, 2024, zilisukumwa hadi jana.
Msemaji huyo wa Serikali amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka mwongozo huo akisema watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Baadhi ya shule hizi zinatumika kama vituo vya uokoaji. Hivyo, zikifunguliwa tena wanatarajia wananchi waliohamishwa waende wapi?.”
Mwaura amesema Serikali inaratibu shughuli ya kuwahamisha wananchi walioathirika ili kutoa makazi ya muda kwa watu waliopoteza makazi yao.
Wakati huohuo duru kutoka nchini humo zimeripoti idadi ya watu waliokufa katika mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo ya Afrika Mashariki imepanda na kufikia watu 228.
Serikali ya nchi hiyo ilibainisha Jumapili kwamba watu tisa walikufa tangu Jumamosi na zaidi ya watu 200,000 wameathirika na 163,000 wamehamishwa hadi sasa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu, mvua za masika zilizoanza kunyesha Machi zimesababisha mafuriko makubwa nchi za Kenya, Tanzania, Burundi, Somalia, Rwanda na maeneo mengine ya Afrika Mashariki.
Mvua za mwaka huu zinatajwa kuwa kubwa kutokana na hali ya El -Nino huku wataalamu wakibainisha kwamba mabadiliko ya tabianchi pia yamezidisha hali ya kujirudia mara kwa mara kwa hali hiyo ya hewa.
(Imeandaliwa na Sute Kamwelwe)