Kocha mpya aifumua Yanga, Moallin …

JUZI tulishuhudia Kocha mpya wa Manchester United, Ruben Amorim akitua klabuni hapo akitokea Sporting Lisbon akiwa na wasaidizi wake watano. Wale aliowakuta akiwemo kocha wa muda, Rud van Nistelrooy akiwapiga chini akisema hawapo katika mipango.

Kitu hicho ndicho kinachokwenda kutokea pale Yanga na mabosi wa klabu hiyo wakiwa bado wamemganda Kocha Mualgeria, Kheireddine Madoui, imebainika mipango yake ni kuja na wasaidizi wawili na kulifumua benchi la ufundi la sasa.

Wakati hayo yakijiri, kuna hesabu za kimyakimya zinaendelea pale Yanga ingawa mabosi wa timu hiyo hawataki kuonyesha kitu lakini uhakika ni bado kocha wao mkuu, Miguel Gamondi hayupo salama kwenye nafasi yake, ndiyo maana mazungumzo ya kumpata mrithi wake yanaendelea huku jina la Kheireddine Madoui raia wa Algeria likikaa mbele zaidi.

Kilichochelewesha dili hilo hadi sasa ni hatua ya kocha huyo kupambana kumalizana na waajiri wake wa sasa CS Constantine ya kwao Algeria na mkataba wake unamtaka ili aweze kuuvunja anatakiwa kutoa notisi ya wiki mbili kabla.

Ugumu anaokutana nao Madoui ni Yanga imekomaa, inamtaka sasa na muda huo wa wiki mbili anatakiwa kuwa ndani ya ardhi ya Tanzania, hatua ambayo kocha huyo imelazimu kuendelea kukomaa na mabosi wake.

Yanga tayari imeshamtumia mkataba kocha huyo na wameshakubaliana atashuka na wasaidizi wake wawili atakaoungana nao kwenye benchi lake jipya huku akiwa tayari tiketi ya ndege anayo kwenye simu yake.

“Sisi tunamsubiria yeye (Madoui) amalizane kwanza na klabu yake, wakikubaliana atakuja haraka hapa na hapo ndipo tutangaza maamuzi mengine ya wale watakaondoka,” alisema bosi mmoja wa juu ndani ya Yanga na kuongeza.

“Upande wetu Yanga tulishamaliza kila kitu, tunajua tunachokifanya, mashabiki wetu wataeleweshwa na wataelewa kwa nini maamuzi hayo tunataka kuyachukua sasa, kuhusu Gamondi kuendelea na kazi ni sawa kwa kuwa kwa sasa bado ni kocha wetu kila mmoja anaendelea na mkataba wake, wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi.”

Kocha Abdihamid Moallin ameendelea kutengeneza mwanzo wake mpya Yanga na juzi alitua makao makuu klabu hiyo kukutana na Ofisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine lakini taarifa mpya ni kwamba atapewa nafasi moja kubwa ya juu.

Awali ilionekana Moallin anayetua Yanga akitokea KMC atapewa nafasi ya kocha msaidizi, lakini mabosi wa Yanga wanapiga hesabu mpya wakitaka awe Mkurugenzi wa Ufundi.

Akili ya Yanga kwenye hesabu hizi ni wanataka kocha huyo aweze kumsaidia Madoui kwenye kujua klabu nyingi za Tanzania, pia kutengeneza ustawi mzuri wa soka la vijana ambalo Mmarekani huyo mwenye asili ya Somalia ana ujuzi nao mkubwa.

Yanga pia imejiweka mguu sawa kuwa kocha huyo hata kama mpango wa kumwondoa Gamondi ukikwama sasa basi kama atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi hakutakuwa na shida ya wawili hao kutoelewana tofauti na kama akitua Yanga kuwa kocha msaidizi.

Related Posts