Hali ilivyo Karimjee mwili wa Mafuru ukiagwa Dar

Dar es Salaam. Waombolezaji wanaendelea kujitokeza kuaga mwili wa aliyekuwa katibu mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru.

Mafuru anaagwa leo Alhamisi, Novemba 14, 2024 kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Katika eneo hilo, waombolezaji wanaingia mmoja mmoja baada ya kukaguliwa kwa mashine getini.

Baada ya ukaguzi, wanatakiwa kupitia sanitaiza na barakoa ndipo kuelekea kuketi.

Kila kiti kilichopo kwenye uwanja huo kuliwekewa maji ya kunywa kwa ajili ya waombolezaji, huku nyimbo za maombolezo zikiendelea.

Mafuru alifariki dunia Novemba 9, 2024 kwenye Hospitali ya Apollo nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mwili wake uliwasili Tanzania Jumanne ya Novemba 12, 2024 na kupokewa na baadhi ya waomboleza walioongozwa na baba yake, Gamba Mafuru na mkewe Noela Mafuru aliyekuwa naye India.

Waombolezaji wakiwa katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam kuaga mwili aliyekuwa katibu mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru.

Katika ibada ya kuaga mwili huo inayoendelea, mwili wa Mafuru umekwishawasili huku viongozi mbalimbali wakiendelea kuwasili kuungana na familia na waombolezaji wengine katika tukio hilo la kuuaga mwili wa mpendwa.

Wakati waombolezaji wakiendelea kusubiri jeneza lenye mwili litakaloingia wakati wowote kuanzia sasa, salamu za rambirambi zimeendelea kutolewa na baadhi ya waombolezaji.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali

Related Posts