Eneo la Kitanzini Wajerumani walipokuwa wakinyonga Wahehe kujengwa makumbusho

Iringa. Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada amesema wanatarajia kujenga makumbusho ili kuhifadhi historia ambako Wajerumani wakati wa utawala wao walikuwa wakiwanyonga Wahehe waliomtii Chifu Mkwawa.

Eneo hilo, inasemekana kulikuwa na mti uliotumika kuwanyongea raia hao wenyeji na kuwa aliyefikishwa hapo alifungwa kitanzi shingoni na kuning’inizwa hadi kufa.

Neno ‘kitanzi’ ndilo lililozaa jina la mtaa na kata – Kitanzini – lilipo eneo hilo la kihistoria.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Ngwada amesema kutokana na historia hiyo wageni wengi hutembelea eneo hilo lenye ‘kitanzi’ ili kulishuhudia.

Amesema kutokana na kuwa kivutio hicho cha utalii, awali walijenga mnara wenye kitanzi lakini bahati mbaya ukawa katikati ya Barabara, kiasi cha kuzuia magari kupita.

“Sasa tunajenga pembeni na wazee wametuonyesha kilipokuwa kitanzi chenyewe, wapo ambao waliuona mti huo. Hapo ndio tutajenga makumbusho,” amesema Ngwada.

Mzee Enus Kalinga, mkazi wa Kitanzini amesema alishuhudia mti huo kabla haujakatwa miaka ya 1950.

“Nimeuona mti na waliukata wakati nimezaa mtoto wa kwanza. Mtu wa kwanza waliyemnyonga ni baba yake Mzee Ngenzi,” anasema Pelda Sekabogo.

Wakazi wa Mtaa wa Kitanzini wamesema makumbusho hayo yatasaidia kutunza historia ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa simulizi zilizopo, Wajerumani waliacha kuwanyonga Wahehe kwenye eneo hilo baada ya kuingia utawala wa Waingereza.

Akizungumzia makumbusho hayo, Mtafiti na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Sanga amesema ni kweli kwamba historia inapaswa kuhifadhiwa.

“Kitanzini ni eneo ambalo huwezi kuacha kulitaja unapoelezea historia ya Mhehe. Wahehe waliomtii Mkwawa waliishia hapa,” amesema Sanga.

Related Posts