Dar es Salaam. Mfanyabiashara Deogratius Tarimo aliyenusurika kutekwa na watu waliojitambulisha kuwa ni Polisi, Novemba 11, 2024, amesema stamina na unene vilimsaidia asiingizwe kwenye gari la watu hao.
Tukio hilo lililotokea Novemba 11, 2024 kwenye Hoteli ya Rovenpic, Kiluvya, jijini Dar es Salaam.
Video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inayowaonyesha watu wawili wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari Tarimo, maarufu Deo Bonge iliyoibua mjadala mitandaoni hususan namna alivyopambana kuzuia asiingizwe kwenye gari.
“Siwezi kusema kama ni mwili moja kwa moja, ila stamina nayo imechangia. Sawa mwili nao umechangia, maana kama sio hivyo ingekuwa rahisi,” amesema Tarimo alipohojiwa na Clouds TV jana Novemba 13, 2024.
Amesema baada ya tukio lile alikwenda kituo cha Polisi Gogoni kuripoti.
“Mimi niko sawa. Nilipokwenda kituo cha Polisi Gogoni walinipa ushirikiano mzuri kabisa na baada ya hapo naendelea vizuri,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 14, 2024, Tarimo ambaye hakutaka kuingia kwa undani kuhusu sakata hilo, amesema mpaka sasa hajawajua waliokuwa wakitaka kumteka.
“Kwa kweli mimi sijaweza kujua mpaka sasa hivi, japo wao Polisi wanakanusha wale sio Polisi. Tuliwahoji walisema wao ni askari maana hata vitambulisho hawakutuonyesha,” amesema.
Hata hivyo, simulizi za mashuhuda wa tukio hilo akiwemo muhudumu wa hoteli hiyo wanaeleza tukio lilivyokuwa na jinsi watu hao walivyofika eneo hilo akidai walijitambulisha ni askari Polisi wa Kituo cha Gogoni wakimtaka apande kwenye gari aina ya Raumu waliyokwenda nayo.
Taarifa zaidi zilizopatikana mitandaoni zimesema kuwa Tarimo alikuwa ana wasiliana na watu waliotaka kumteka tangu Oktoba 25, 2024 na walielewana wakutane Jumatatu Novemba 11, 2024 kwa maelewano ya kibiashara.
Alipoulizwa kama alikuwa akiwasiliana na watu hao kabla ya kukutana nao, Tarimo amesema mambo mengine yako kwenye uchunguzi wa Polisi.
“Ni kweli, lakini sasa haya mambo yako kiuchunguzi na yapo chini ya Polisi nafikiri ngoja tuache wayakamilishe halafu ndio iwe rahisi kutoa taarifa kamili, kwa sababu kutoa taarifa mbilimbili zinaweza kukinzana.
“Taarifa ya awali ndio ile niliyoitoa na wao wameitoa, lakini ngoja hao wakamilishe halafu tutatoa taarifa iliyokuwa sahihi zaidi,” amesema.
Taarifa hizo zinadai kuwa familia anayotoka ni ya wafanyabiashara na awali walikuwa wakimiliki baa zenye jina la Sunset na sasa anamiliki maduka manne ya vifaa vya ujenzi (hardware).
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu biashara na familia yake amesema, hayo ni mambo binafsi.
Jana, Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake, David Misime limetoa taarifa kwa umma likieleza kufuatilia na kuahidi kuwakamata watu hao.