Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema ni muhimu kuhakikisha fedha za ufadhili wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinawafikia wazawa ili waweze kubuni miradi ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuwa wanafahamu zaidi changamoto za maeneo yao.
Dk Mpango anayasema haya akisisitiza uwajibikaji wa nchi zilizoendelea kutoa fedha kwa nchi zinazoendelea ili kukabiliana na athari za mabadikiko hayo.
Hata hivyo, fedha za ufadhili zilizotolewa ahadi ya kila mwaka kutoka nchi zilizoendelea zikiwa ni Dola 100 bilioni ambazo ni zaidi ya Sh250 trilioni ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ameyasema hayo wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kukabidhi tuzo kwa kwa washindi wa miradi ya ubunifu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa na jamii za asili (wazawa) kutoka sehemu mbalimbali duniani katika shindano linaloratibiwa na Taasisi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Duniani (GCA).
Hafla hiyo imefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.
“Tanzania inaendelea na uwekezaji ili kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala kama vile jotoardhi, nishati ya jua na upepo huku ikiendelea kukabiliana na nishati chafu ya kupikia ambayo imekua chanzo cha ukataji miti na upotevu wa hifadhi ya kaboni inayopelekea uharibifu wa rasilimali za kijani,” amesema.
Dk Mpango amesisitiza umuhimu wa viongozi kuwatambua na kuwawezesha wabunifu wa miradi inayotekelezwa na wanajamii wa asili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha ametoa wito kwa jamii kuendelea kuanzisha miradi ya ubunifu itayosaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Taasisi ya GCA kuongeza wigo wa mashindano hayo ili kuwafikia wabunifu wengi zaidi ikiwemo wanaofanya shughuli zinazohusiana na uchumi wa buluu.
Amesema Tanzania ina mifano ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutoka kwa wananchi wazawa ambapo wanawake katika ukanda wa bahari Zanzibar wanajishughulisha na kilimo cha mwani ambacho ni matokeo ya kuongezeka kwa kina cha bahari kunakosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania ambayo ni miongoni mwa washiriki imeazimia kuwa na mikakati ya pamoja na nchi wanachama ikiwa ni hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoshuhudiwa maeneo mbalimbali duniani.
Mshauri wa nishati mpito Afrika kutoka Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’ anasema dhana ya fedha kuwafikia wazawa ni nzuri amesema jambo la msingi ila inahitaji uratibu wa kuwafikia walengwa halisi.
“Uratibu wa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha azma hiyo inafikiwa. Amesema kuliko fedha hizo kupitia mikono mingine ni jambo jema kama zitafika moja kwa moja kwa wahusika,” amesema Olang’.
Aidha amesema katika kuhakikisha fedha za wafadhili zinatolewa kwa wakati amesema inahitajika sauti na nguvu ya pamoja ambayo itaeleta ushawishi kwa wafadhili kutimiza ahadi zao.
“Nchi zinazoendelea zinapaswa kuwa na sauti ya pamoja kuweza kuwafanya walioendelea wanatimiza ahadi zao ingawa kuna mashaka kama watatimiza kwa asilimia miamoja,” amesema.
Mdau na Mwanaharakati wa Mazingira, Clay Mwaifwani amesema ni suluhisho ijapokuwa mabadiliko ya tabianchi kuwa na athari za muda mrefu hivyo suala la kupewa fedha linapaswa kuendana na kujengewa wazawa uwezo wa shughuli wanazozifanya kulingana na mabadiliko hayo.
Amesema fedha zitolewe ingawa zinasuasua kutoka kwa wafadhili ila amesema ijengwe utaratibu kwa wazawa namna ya kukabiliana na athari hizi ikiwemo wakulima.
“Wakijengewa uwezo wa kupambana itakuwa jambo la msingi zaidi kwani fedha huisha. Ila uwezo utafanya kilimo kiwe himilivu,” amesema.
Kuhusu suala la bunifu amesema ni wazo zuri kwani nchi za zinazoendelea zina uwezo mdogo wa kukabiliana na mabadiliko hayo hivyo suala la bunifu linapaswa kushikiliwa kwa namna ya kuwa na watu wengi.
Amesema ubunifu unahahakishwa unawanufaisha watu wengi na kuwafikia watu wengi kila siku kuweza kupambana na mabadiliko ya tabianchi.