ILE Yanga sio timu yenye rafiki au adui wa kudumu. Muda wowote unaweza kuwa rafiki yao na dakika sifuri wanaweza kukugeuka ukawa adui wao.
Mchezaji kipenzi pale Yanga kwa siku za hivi karibuni ni Stephane Aziz Ki kutokea Burkina Faso ambaye anapendwa kweli kuanzia na mabosi hadi na mashabiki wa timu hiyo.
Ule mkataba mnono aliosaini miezi michache iliyopita hadi akazua mjadala hapa kijiweni ni ishara tosha ya mahaba ambayo Wanayanga wamekuwa nayo kwa Aziz Ki.
Hili ni jambo lililo wazi, Yanga ikishampenda mchezaji, huwa haikubali kirahisi aondoke iwe kwa kwenda nje ya nchi au timu tofauti humu ndani na watatumia kila aina ya ushawishi ili abaki hata kama kwa hela ya kukopa au kujichanga.
Sasa kuna maneno yanaendelea mitaani huku kuwa Aziz Ki hivi sasa sio yule ambaye Wanayanga walimuona msimu uliopita na wanadai hadi sasa tangu msimu umeanza hajawatimizia kile walichokitegemea kwake.
Wanakumbuka alikuwa mchezaji bora na mfungaji bora hivyo tamaa yao ni kuona anakuwa na muendelezo wa pale alipoishia ili wasianze kupata wasiwasi pesa ndefu ambayo wamempa ili asaini mkataba imeanza kutumika kihalali na sio kama walimpa tu.
Kuna jamaa hapa yeye anasema anatamani zaidi Aziz Ki aonyeshe makali yake hivi sasa ili amfunike yule dogo wa Simba aliyetoka Ivory Coast ambaye kwa sasa ndiye anaongoza kwa kuhusika na idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi Kuu.
Anaona kama dogo asipopata upinzani mapema anaweza kupata konfidensi zaidi ambayo itamfanya azidi kuwa tishio na mwisho wa msimu akafanikiwa kuichukua kwa mara ya pili tuzo aliyoipata msimu uliopita huko Ivory Coast hadi Simba ikaamua kuvunja benki kumnasa.
Aziz Ki inabidi apambane sana hivi sasa ili awafanye Yanga waendelee kutamba mtaani. Hawakawii kumgeuzia kibao wakiona anawazingua maana huwa kwao timu kwanza mtu baadaye.