Sababu zinazompa Kibu thamani | Mwanaspoti

Kibarua kigumu ambacho Simba inacho katika kumbakisha nyota wake Kibu Denis anasaini mkataba mpya kinachangiwa na ufanisi wa mchezaji huyo uwanjani licha ya kutokuwa na takwimu bora za kuhusika na mabao, thamani ya mkataba wake uliopita lakini pia uwepo wa ofa nono mezani kutoka timu nyingine.

Licha ya mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza vyema nafasi ya winga na mshambuliaji wa kati kutokuwa na takwimu nzuri msimu huu katika kupika na kufunga mabao, amegeuka gumzo hivi sasa kutokana na taarifa za kutosaini mkataba mpya wa timu hiyo wakati ule wa sasa ukifikia tamati mwishoni mwa msimu huu, yaani baadaye mwezi huu.

Kwa hapa ndani, Kibu Denis ana ofa za mkataba wa Simba inayotaka kuendelea kubaki naye, Yanga na Ihefu huku pia kukiwa na timu mojawapo inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri ambayo nayo inamtaka winga huyo ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa ya kulinda anapotokea pembeni.

Meneja anayemsimamia mchezaji huyo, Carlos Sylivester ameweka hadharani kile ambacho Kibu anakihitaji ili abakie Simba ama ajiunge na timu nyingine kuwa ni dau la usajili lisilopungua Sh 400 milioni na mshahara usiopungua Sh 15 milioni na upande utakaokuwa tayari kufikia kiasi hicho itamnasa kirahisi winga huyo aliyewahi kuwika akiwa na Mbeya City.

“Huyu ni mchezaji ambaye anategemea mpira kwa ajili ya kuendesha maisha yake na kwa sasa mahitaji yetu ndio hayo. Tunachohitaji ni maslahi bora kwa upande wake ili naye afanya kazi bora akiwa uwanjani,” alisema meneja huyo.

Mahitaji hayo ya Kibu Denis yanakuja katika kipindi ambacho mchezaji huyo amefunga bao moja tu katika Ligi Kuu msimu huu huku akiwa hajafumania nyavu kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini kuwa kitendo cha Kibu kuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Simba chini ya makocha tofauti pamoja na timu ya taifa ‘Taif Stars’, ni miongoni mwa sababu zilizochangia kupanda kwa thamani yake sokoni na makocha wa timu nyingine kutaka kumuona akitumika kwao.

Uwezo mkubwa wa kukaba kuanzia mbele timu inapopoteza mpira pamoja na nishati aliyonayo inayomuwezesha kushinda mapambano mengi ya kuwania mpira na wachezaji wa timu pinzani, vimefanya Kibu awe lulu katika kikosi cha kwanza cha Simba pamoja na kukaukiwa na mabao.

Sifa hizo zinaonekana kuwa kipaumbele cha makocha wengi katika soka la kisasa jambo linalompa fursa Kibu kupata muda wa kutosha wa kucheza kikosini.

Katika Ligi Kuu msimu huu, Kibu Denis amecheza mechi 21 kati ya 23 ambazo Simba imecheza hadi sasa ambapo kati ya mechi hizo, mechi 17 alianza katika kikosi cha kwanza na nne aliingia akitokea benchi.

Michezo miwili ambayo amekosa dhidi ya Namungo na dhidi ya Mtibwa Sugar jana yote akiwa anasumbuliwa na majeraha majeruhi.

Kibu kudhihirisha kuwa amekuwa muhimu kwenye kikosi cha Simba, katika Ligi ya Mabingwa Afrika, amecheza mechi zote 10 msimu huu kuanzia zile za hatua ya awali hadi robo fainali ambapo mechi tisa ameanza katika kikosi cha kwanza na mchezo mmoja aliingia akitokea benchi.

Mchezaji wa zamani Simba Dua Said alisema Kibu Denis ni mchezaji kama walivyo wengine ila utofauti wake bado ni mkubwa licha ya kuwa hana rekodi nzuri tangu alipoifunga Yanga bao moja katika mchezo wa kwanza.

“Ni mchezaji ambaye hawezi kukosa timu na makocha wengi wanamkubali kwa sababu ni kiungo mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa na juhudi ya kupambania timu hasa akiwa uwanjani ni ngumu kumpata mchezaji ambaye muda huohuo anakusaindia kuzuia, wakati huohuo anakuwa na pumzi ya kushambulia, hiki ndiyo makocha wengine wanataka,” alisema Dua.

Kipa wa zamani Simba Hussein Sharrif ‘Casillas’ alisema, Kibu kinachompa thamani ni kucheza kwa ajili ya timu na kufuata vyema maelekezo ya makocha.

“Ni miongoni mwa wachezaji wazawa wachache wenye mioyo ya kujitolea kwa ajili ya timu na kujitambua licha ya kuwa hana rekodi nzuri hilo sio tatizo kwani kufunga sio tatizo lakini kusababisha timu kupata matokeo ndio jambo la muhimu tazama hata timu ya taifa amekuwa akiitwa kutokana na ubora wake,” alisema Casilas.

Sababu ya pili ambayo inaonekana kumpandisha thamani Kibu ni fedha aliyopata wakati anasaini mkataba unaomalizika wa Simba ambapo usajili wake uligharimu kiasi kinachokadiriwa kufikia Sh 200 milioni, jambo ambalo anaamini linatakiwa kutokea tena leo.

Kana kwamba haitoshi, sababu ya tatu ni timu za Ihefu na Yanga kuonekana kuwa tayari kumlipa mchezaji huyo mshahara wa Sh 15 milioni kwa mwezi ambao anauhitaji huku kila moja ikionekana kuwa na utayari wa kulipa kiasi cha Sh 300 milioni kama dau la usajili ni uzoefu wake kwenye ligi na umri wake.

Kibu ameshacheza Ligi Kuu Bara zaidi ya misimu minne akiwa na kiwango bora akiwa na timu za Geita na Mbeya City, lakini pia uhabu wa wachezaji bora wazawa kwa sasa ni sababu nyingine.

Related Posts