Geita. Wananchi wa Kata za Mtakuja na Kalangalala katika Halmashauri ya Mji wa Geita wamedai maisha yao yako hatarini kutokana na uwepo wa makundi ya nyani yanayoingia kwenye makazi yao kuchukua vyakula na kuzua hofu zaidi kwa watu wenye watoto wachanga.
Wamedai kumekuwa na ongezeko kubwa la nyani wanaotokea kwenye msitu unaozunguka mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) na kuingia kwenye makazi yao na pindi mtu anapoacha mlango au dirisha wazi, nyani hao bila woga huingia ndani ya nyumba na kuiba chakula.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Musa Nyaronyo mkazi wa Mtaa wa Kagera na Eveline Sabuka, mkazi wa Mtaa wa Compaund, wamesema nyani hao huvamia mara kwa mara kwenye makazi yao na kuhatarisha usalama wa maisha hasa ya watoto na kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuwaua kabla hawajasababisha madhara kwa binadamu.
“Sasa hivi mtoto akilala lazima uwe karibu, unapata hofu asijekubebwa na nyani. Mfano juzi hapa nyumbani kwangu waliingia kundi la nyani zaidi ya sita, walipokuta nje hakuna kitu, nimekaa ndani naona wanaingia, hawana hata hofu, wanaparamia ugali. Nilishangaa maana ni tukio la ajabu nyani anafanya vitu kama binadamu,” amesema Nyoronyo.
Diwani wa kata ya Kalangalala, Prudence Temba amedai hali ni mbaya kwenye kata yake na hatua za dharura zinahitajika za kuwahamisha au kuwaua nyani hao kwa usalama wa wananchi.
Ofisa Maliasili katika halmashauri hiyo, Lee Kiangala amezungumzia sababu za nyani kuvamia makazi ya watu akisema sababu kuu ni uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji wa miti katika msitu wa Geita.
Amesema msitu wa Geita wenye hekta zaidi ya 50,000 umeharibiwa kabisa kwa shughuli za kibinadamu na kusababisha wanyama waliokuwa kwenye msitu huo kuhamia kwenye msitu wa GGM na sasa wanatokea kwenye msitu huo na kuingia kwenye makazi ya watu.
“Msitu wa Geita umeharibiwa sana na eneo lililobaki lenye msitu ni la GGM ambalo lina ulinzi, sio rahisi wananchi kuingia na nyani walihamia huko na sasa wamekuwa wengi wanatoka na kuingia kwenye makazi ya watu hasa kwenye mitaa ya Ikumbayaga, Nyamalembo, Nyanza na Mkoani, kero ni kubwa,” amesema Kiangala.
Ili kumaliza changamoto hiyo, amesema tayari wamewasiliana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) ili kuwahamisha nyani hao na kuwapelekea kwenye hifadhi ya Moyowosi.
Amesema shughuli ya kuwahamisha nyani hao itaanza hivi karibuni na itafanyika kwa siku 17, amewataka wananchi kutunza mazingira na kuepuka kukata miti ovyo kunakosababisha wanyamapori kusogea kwenye makazi ya watu.