Mdogo wa Mafuru aeleza dakika za mwisho za kaka yake hospitalini

Dar es Salaam. Maendeka Mafuru ambaye ni mdogo wa Lawrence Mafuru ameeleza saa za mwisho za kaka yake akiwa anapigania uhai katika Hospitali ya Apollo, nchini India zilivyokuwa.

Mafuru (52) alifikwa na mauti Ijumaa ya Novemba 9, 2024 kwa ugonjwa wa saratani ya damu na mwili wake umeagwa leo Alhamisi, Novemba 14, 2024 katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na waombolezaji mbalimbali akiwemo, Rais Samia Suluhu Hassan.

Akitoa salamu za familia kwenye shughuli hiyo, Maendeka ambaye amezungumza kwa huzuni akijizuia kulia, amesema kaka yake alipata huduma ya kiroho saa chache kabla ya kifo chake.

“Sisi Waadventista katika imani yetu ya Kisabato, Biblia inasema mkiona mtu amefika hatua ya mwisho, waite wazee wampake mafuta, ndicho tulikifanya kwa kaka yetu kule India,” amesema.

“Siku ya Ijumaa (Novemba 8) saa chache kabla ya kifo chake tulipata huduma hiyo kutoka kwenye Kanisa la Waadventista Wasabato la New Delhi, India.”

Maendeka ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya wanne kwenye familia ya kina Mafuru ambaye ndiye kijana mkubwa, ametoa shukrani za familia na kumshukuru Rais Samia ambaye ni miongoni mwa waombolezaji kwenye tukio la kuaga linalofanyika kwenye uwanja wa Karimjee.

Amesema, wakiwa nchini Tanzania na hata baada ya kumpeleka ndugu yao India, madaktari walijitahidi kuokoa uhai wa Mafuru, lakini Mungu alipenda alale usingizi wa mauti.

“Tulipata ushirikiano mkubwa, nchini India ubalozi wa Tanzania kule ulitupa ushirikiano, kuna nyakati Mafuru aliletewa vyakula vya Kitanzania hospitali na alivifurahia,” amesema.

Miongoni mwa salamu ambazo amezitoa na kumfanya kutokwa machozi ni pale alipoishukuru Benki ya NMB anapofanya kazi (Mahendeka) kumruhusu kwenda kumuuguza kaka yake. Akielezea hivyo, alisita na kutokwa machozi na mtu aliyekuwa amesimama kando alisogea na kumshika begani.

Maendeka amesema kwa kuwa yeye ni mtoto wa pili kuzaliwa na kaka yake amefariki, ameiomba familia kumwombea ili aweze kuwaongoza kwa kuvaa viatu vya kaka yake. Mafuru ameacha mke na watoto wawili wa kike.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Related Posts