Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafungia leseni za udereva madereva sita kwa makosa ya kuendesha wakiwa wamelewa, mwendo wa kasi na kupita magari yaliyo mbele yao bila kuchukua tahadhari.
Jeshi hilo limewataka madereva hao warudi vyuoni kwa ajili ya mafunzo zaidi ya udereva ili kuwa na uelewa wa vihatarishi vya ajali. Katika madereva hao sita, wamo madereva watano wa mabasi ya abiria.
Taarifa iliyotolewa jana Novemba 13, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, imetaja makosa mengine kuwa ni kuzidisha abiria, kuendesha gari kwa njia ya hatari na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.
Miongoni mwa ajali zilizotokea hivi karibuni jijini Mwanza ni ile ya Oktoba 22, 2024 iliyoua watu tisa na wengine 39 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Nyehunge, lililokuwa likitokea Morogoro kwenda mkoani Mwanza, kugongana uso kwa uso na basi la Asante Rabi lililokuwa likitokea Mwanza kwenda jijini Arusha, chanzo kikiwa ni mwendo wa kasi na dereva wa basi la Asante Rabi kutaka kulipita gari jingine bila tahadhari.
Ajali nyingine ilitokea Agosti 4, 2024 ambapo abiria 45 walinusurika kufariki dunia baada ya basi la Kampuni ya Bunzali Mtoto Safaris kupinduka eneo la Buhongwa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Kwa mujibu wa Mutafungwa, madereva waliofungiwa leseni ni Abas Said (38), dereva aliyekukuwa akiendesha basi la Kampuni ya Ally’s akiwa amelewa, Gereon Luyendela (53) aliyekuwa akiendesha basi la Kampuni ya Ally’s kwa njia ya hatari na kuyapita magari mengine sehemu iliyokatazwa bila kuchukua tahadhari.
Wengine ni Anwari Mohamed (44), aliendesha basi la Kampuni ya Nyehunge kwa njia ya hatari bila kujali watumiaji wengine wa barabara kwenye eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu, Machage Mikwabe (42) aliyeendesha basi mali ya Kampuni ya Katarama na kunyang’anywa leseni kwa kosa la kuyapita magari mengine sehemu isiyoruhusiwa ya makazi ya watu.
Pamoja na Farouk Melimeli (46), aliyekuwa akiendesha basi, mali ya Kampuni ya Frester kwa kosa la kuendesha mwendo wa kasi na Masalu Manyirizi (35), mkazi wa kadashi aliendesha gari aina ya Probox akiwa amezidisha abiria.
“Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa kuwataka madereva wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuacha kufanya matendo hatarishi yanayoweza kusababisha ajali,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Wapo baadhi ya madereva hususani wa magari ya kubeba abiria wameendelea kupuuza elimu hiyo wanayoipata kutoka kwa askari wa usalama barabarani na kufanya makosa hatarishi ambayo yanaweza kusababisha ajali.”