Bashungwa asimulia alivyosotea hati ya ardhi kwa miaka mitatu Karagwe

Karagwe. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuboresha utaoji huduma wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ili litende haki wakati wa usuluhishi wa migogoro na kupunguza malalamiko ya wananchi ili kukomesha migogoro ya ardhi.

Bashungwa ametoa rai hiyo Jumatano, Novemba 13, 2024 Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25 kilichohusisha watendaji wa halmashauri na kata.

Amesema ameshuhudia utendaji mbovu wa baraza la ardhi katika Wilaya ya Karagwe kwa sababu hata yeye ni mwathirika kwa maana amesota zaidi ya miaka mitatu kutafuta hati yake bila mafanikio, hivyo ameitaka halmashauri itupie jicho na kuboresha mifumo ya utoaji huduma.

Amelitaka baraza la ardhi kupunguza malalamiko ya wananchi kwa kuwa mabaraza ya ardhi yanapochelewesha haki kwa kumzungusha mwananchi, ni gharama kubwa na yanatia umasikini.

Bashungwa ameitaka halmashauri kufanya tathimini ya utoaji huduma kwa baraza hilo ili kujua changamoto zinazokwamisha utoaji wa haki kwa wakati na wanaohusika kukwamisha wachukuliwe hatua.

Ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kujikita katika mipango miji na upimaji wa ardhi katika maeneo yanayoendelea kukua ili kuendana na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ili kuepusha migogoro ya ardhi kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Wallace Mashanda amemhakikishia Waziri Bashungwa kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa na watafanya kila linalowezekana huduma na mifumo iboreshwe.

Pia, amewasisitiza madiwani kuendelea na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yanayowazunguka kwa kuendelea kupanda miti kwa wingi.

Mkazi wa kata ya Kayanga, wilayani Karagwe, Waida Abdul amesema mara nyingi amekuwa akiona watu wakiteseka katika ufuatiliaji wa huduma ya kupata hati za viwanja kwenye mabaraza ya ardhi, hivyo anaomba Serikali kupitia upya kanuni na sheria za kupata hati hizo.

Related Posts