Geita. Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Costantine Morand, ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza ujenzi wa lambo la maji linaloendelea kujengwa katika Kata ya Nyanguku kwa gharama ya Sh64 milioni.
Ombi hilo linatokana na malalamiko ya Diwani wa Nyanguku, Elias Ngole aliyedai kuwa mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2022 kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), lakini hadi sasa haujakamilika na fedha zimekwisha.
Akizungumza katika kikao cha baraza hilo tkilichofanyika jana Jumatano Novemba 2024, Diwani Ngole amesema Tasaf ilitenga Sh64 milioni kwa ajili ya mradi huo na Sh30 milioni zilitengwa kwa ajili ya malipo ya vibarua ambao ni walengwa wa Tasaf, Sh33 milioni kwa ajili ya ujenzi wa lambo na Sh1 milioni kwa ajili ya usimamizi.
Ameogeza kuwa, mtambo wa kuchimba ulioletwa ulikuwa mbovu na ulipelekwa baada ya wiki mbili bila kutumika, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa mradi na matumizi ya fedha kumalizika bila mradi kukamilika.
Ngole amesema baada ya kulalamika katika mabaraza yaliyopita, waliosimamia mradi huo walianza kurejesha fedha na kuweka Sh2 milioni, kisha Sh6 milioni, ambazo sasa wanataka zitumike kumalizia ujenzi hu.
Ameeleza shaka yake kwa kusema, “Kama wameshindwa kukamilisha mradi kwa Sh20 milioni, hiyo Sh8 milioni itasaidia nini?”
Pia, amedai kuwa malipo hayo yameanza kuwekwa katika akaunti ya kata na akaunti binafsi, awali Sh2 milioni ziliwekwa na baadaye Sh8 milioni.
Mratibu wa Tasaf wa Halmashauri ya Mji Geita, Amani Madenge amesema alikabidhiwa mradi huo wakati utekelezaji ulikuwa umeshaanza na alithibitisha kuwa mradi huo ulitengewa Sh64 milioni na asilimia 50 ya fedha hiyo ilikuwa kwa ajili ya malipo ya walengwa wanaofanya kazi kwenye mradi huo.
Amesema Sh34 milioni zilikuwa kwa ajili ya walengwa, Sh20 milioni kwa ajili ya mitambo na Sh10 milioni kwa ajjili ya vifaa huku akikiri kuwa lambo hilo ni kubwa na fedha iliyotengwa haitoshi, hivyo walianza ujenzi ili kuepuka fedha kurudi Tasaf.
Amesema lambo hilo lilichimbwa kwa gharama ya Sh20 milioni kwa hatua ya awali, tofauti na hali yake ya sasa baada ya mvua kunyesha, ambapo tayari limeota nyasi.
Amebainisha kuwa hatua za awali zilifanywa kwa utaratibu unaofaa chini ya usimamizi wa wahandisi na wataalamu wa idara ya kilimo.
“Mwalimu wa mradi amesema mtambo ulikuwa na changamoto, hivyo utekelezaji wa mradi haukuendelea kama ulivyopangwa na mvua iliponyesha ikasababisha usumbufu kwenye mpango mzima wa ujenzi wa lambo hilo. Kutokana na fedha kutotosheleza, tuliomba nyongeza kutoka Tasaf ambao walikubali na kuidhinisha Sh8 milioni zaidi.
Hata hivyo, fedha hizo zilipotolewa, mvua ilikuwa inaendelea kunyesha, hivyo tukazihifadhi kwenye ofisi ya Kata kusubiri mvua iishe ndipo tuanze utekelezaji,” ameeleza.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Yefred Myenzi, ameomba muda ili aweze kupitia na kutathmini maendeleo ya mradi huo na kutoa taarifa katika kikao cha kamati ya fedha.
Awali, Mwenyekiti wa baraza hilo, Constantine Morandi akifunga kikao hicho, alimtaka Mkurugenzi kufuatilia na kuwasilisha taarifa ya kamati ya fedha, huku akizihimiza taasisi zinazohusika na uchunguzi kuchunguza utekelezaji wa mradi huo.