Nilipata nafasi na baraka ya kumfahamu Mafuru katika nyadhifa zake kama Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Kamishna wa Sera, Naibu Katibu Mkuu wa Hazina anayehusika na Usimamizi wa Uchumi katika Wizara ya Fedha, na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango. Alikuwa kiongozi mwenye upeo wa hali ya juu, mtu mwenye maono na aliyetumikia nchi kwa moyo mkunjufu na juhudi isiyo na kikomo.
Tulipopata habari za kifo chake, kwenye salamu za rambirambi na kumkumbuka nilikutana na picha ya Mafuru akiwa ameshika kitabu cha Who Will Cry When You Die? kilichoandikwa na Robin Sharma.
Kitabu hiki ni mwongozo unaojenga uongozi wa kiroho na kimaadili kwa mtu yeyote anayetamani kukumbukwa kwa kuacha urithi wa thamani yaani ‘legacy’. Lawrence alikuwa mpenzi wa kusoma, na mara kwa mara alikuwa akitoa mistari na falsafa mbalimbali kutoka vitabu anavyosoma kwa marafiki zake. Kupitia kitabu hiki, Sharma anazungumza kuhusu maana ya uongozi, urithi wa kipekee wa mtu, na umuhimu wa kuishi kwa lengo. Kuona picha ya Lawrence akiwa na kitabu hicho, ilinifanya nifikirie kuhusu uongozi wake na jinsi alivyogusa maisha yangu na ya wengi kwa muktadha wa masomo ya Sharma.
Katika kitabu cha Sharma, kuna fundisho muhimu kuhusu kuishi maisha yenye lengo. Maana halisi ya maisha si katika mali au heshima, bali ni namna ambavyo tunaweza kuacha urithi wenye thamani kwa jamii. Lawrence aliishi maisha yenye lengo, na katika nafasi zake nyingi za uongozi alionyesha uzalendo wa kweli. Aliamini katika kutumikia taifa na kuwa na maono ya siku zijazo. Kama Sharma alivyoeleza, mafanikio ya mtu ni juu ya kuishi kwa njia inayosaidia watu wengine, na Lawrence alithibitisha hilo. Nakumbuka aliposimama kidete na kutoa ushirikano kuanzisha mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) akiamini kwamba sekta ya kilimo inaweza kuwa chachu ya maendeleo. Kwa dhamira hiyo, alifanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbinu za kisasa, na matokeo yake yanaonekana leo kupitia fedha alizoweza kuzipigania kwa ajili ya mradi huo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Ujasiri wa kuthubutu na kujenga tabia chanya
Lawrence alikuwa na ujasiri wa kuthubutu kama ambavyo Sharma anafundisha. Katika maisha yake, hakuogopa kujaribu mawazo mapya kwa ajili ya manufaa ya umma, hili alilidhihirisha pale ambapo aliungana na falsafa ya kiujamaa wakati ilikua inajulikana dhahiri ni mwanamasoko na anayeamini katika ubepari na maendeleo ya kiuchumi.
Katika nafasi yake kama Katibu wa Tume ya Mipango, alisisitiza sana umuhimu wa teknolojia ya kilimo na alisaidia kufanikisha mpango wa Vituo vya Pembejeo na Zana za kisasa za kilimo yaani ‘Mechanization Centers’, ambao umeleta matrekta zaidi ya 10,000 nchini kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wadogo. Lawrence alikuwa kati ya wale walioamini kuwa wakulima hawahitaji kumiliki matrekta bali wanahitaji mashamba yao yaweze kulimwa kwa ufanisi. Katika kila changamoto aliyokutana nayo, Lawrence hakuwahi kukata tamaa wala kuchukua njia rahisi, bali aliweka juhudi na matumaini, akijua kwamba kazi yake ni urithi wa kweli kwa taifa.
Kujenga mahusiano na kuunganisha watu
Sharma pia anaongelea umuhimu wa kujenga madaraja na mahusiano. Lawrence alijua kuwa hakuna mafanikio bila mshikamano na ushirikiano. Alikuwa na juhudi za kipekee za kuunganisha watu kwa pamoja kwa ajili ya malengo makubwa ya taifa. Alikuwa na moyo wa ukarimu, na alitumia nafasi yake ya uongozi kuhimiza mshikamano miongoni mwa watumishi wa umma na wananchi. Lawrence aliwafikia watu kwa lugha yao na kuwahamasisha. Alikuwa na kipaji cha kuleta pamoja watu tofauti, hata wale walio na mitazamo inayotofautiana. Kupoteza mtu kama Mafuru ni pigo kubwa kwa familia, marafiki, na kwa taifa lote.
Katika mazungumzo yetu ya mwisho mnamo Oktoba 10,2024 Lawrence alisikika kama mwenye matumaini, akiamini kwamba angepona. Hata wakati huo wa maumivu, alikuwa na imani kubwa juu ya mustakabali wa sekta ya kilimo nchini Tanzania. Tulijadili mambo mengi ikiwemo ndoto yetu ya kukuza sekta hiyo kwa asilimia 5 ifikapo mwaka 2025, na kwa heshima ya kazi aliyoifanya, nimejitoa kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.
Lawrence, ndugu yangu, imechukua siku kadhaa kutafakari juu ya maisha yako—maisha yaliyojaa uaminifu, weledi, na urafiki wa kweli. Leo, tunaomboleza kifo chako na kujiuliza maswali mengi. Ulikuwa mtu wa kujitolea na mfanyakazi hodari. Kama Waziri wa Kilimo, nitakukumbuka milele kwa hatua tulizochukua pamoja kuboresha sekta hii.
Nuru ya yale uliyoyafanya itaendelea kutuongoza na kututia nguvu kwa siku zote zijazo.
Ninakumbuka kwa mengi ndugu yangu Lawrence, mazungumzo yetu ya kila mara pale ofisini au nyumbani kwako Dodoma. Zilikuwa ni jioni za mazungumzo yenye kina, zilizopanua upeo wangu na kunipa mtazamo mpya juu ya mambo kadha wa kadha. Kila mara ulikuwa na unatutania mimi na Profesa Kitila Mkumbo juu ya kupitwa na wakati hata ki-mavazi, ulituhimiza tuhakikishe kilimo kina “mvuto” zaidi, na jinsi kinapaswa kuwa cha kuvutia zaidi kwa vijana. Ulisisitiza kwamba sekta ya kilimo lazima iwe ya kisasa na tukubali kuangalia masoko kwa mtazamo wa kisasa. Hukusita kutuambia kuwa tulipaswa kuachana na baadhi ya fikra za kijamaa na kufikiria zaidi kuhusu uchumi unaoelekezwa na masoko.
Mazungumzo yetu yameacha alama isiyofutika katika mawazo yangu. Hasa, nitakumbuka jinsi ulivyonipa changamoto ya kutafakari dhana ya kijamaa huku ukinisukuma nizingatie pia kanuni za ubepari. Hakika, ulivunja baadhi ya mitazamo yangu ya zamani na kunionyesha mwanga mpya.
Lawrence, tutakulilia na tutakukumbuka kwa yale yote uliyotufunza. Kama Qur’an inavyosema katika Surat Ali Imran – 3:185 – Kila nafsi itaonja mauti. Asante kwa maono yako, mwongozo wako, na kwa jinsi ulivyotugusa kwa upendo na uongozi wako thabiti. Mwenyezi Mungu akulaze mahali pema peponi, rafiki yangu na kiongozi mwema, Lawrence Mafuru.
Mwenyezi Mungu akulaze mahali pema peponi, rafiki yangu Lawrence.
Na Hussein Mohammed Bashe (MP)
Waziri wa Kilimo – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.