Mkutano wawekezaji sekta ya madini kukutanisha washiriki 1,500

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Washiriki 1,500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kushiriki katika mkutano wa sita wa wawekezaji katika sekta ya madini Tanzania unaotarajiwa kufanyika Novemba 19 hadi 21 mwaka huu.

Mkutano huo utakaofunguliwa Novemba 19,2024 na Rais Samia Suluhu Hassan una kaulimbiu isemayo ‘Uongezaji thamani madini kwa maendeleo ya kuchumi na kijamii’.

Akizungumza leo Novemba 14,2024 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema mada nane zitajadiliwa katika mkutano huo ambapo watoa mada ni wabobezi katika sekta ya madini ndani na nje.

“Mkutano huu ni jukwaa la kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana maarifa, ujuzi na kuangalia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hii inayokua kwa kasi.

“Unatoa fursa kwa washiriki kujifunza kuhusu sera na mikakati mipya ya Serikali, kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na madini na kushuhudia teknolojia mpya na ubunifu unaoweza kuleta thamani zaidi katika utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani madini,” amesema Mavunde.

Amesema mkutano huo utaweka msingi thabiti wa ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini na kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania kiuchumi na kijamii.

Waziri Mavunde amesema katika mkutano huo pia kutakuwa na hafla ya usiku wa madini yenye lengo la kutambua mchango wa wadau waliofanya vizuri katika sekta hiyo kupitia makundi mbalimbali.

Aidha amesema kutakuwa na onesho la bidhaa za madini ya vito, viwandani na ujenzi kwa lengo la kuonesha fursa zilizopo na kutambua matumizi ya madini katika maisha ya kila siku ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa kwa sasa ni asilimia 9 na malengo ni kufikia asilimia 10 mwaka 2025.

Washiriki wa mkutano huo ni pamoja na mawaziri wa madini kutoka nchi za Afrika, watendaji wakuu wa kampuni kubwa za madini zilizowekeza na zinazotarajia kuwekeza nchini, watafiti, mabalozi 31 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje.

Wengine ni mashirika ya kimataifa, waongezaji thamani madini, wafanyabiashara, taasisi za fedha, vyuo vikuu na vya kati, taasisi za umma na binafsi na viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka wizara, taasisi, mikoa, halmashauri na idara za serikali.

Related Posts