Dar es Salaam. Wakati idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ikiongezeka, wasimamizi wa taasisi hilo wametakiwa kuhakikisha taratibu zote za utoaji elimu zimetakiwa kufuatwa bila kupindishwa.
Msisitizo huo unalenga kuhakikisha viwango vya ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi ya vyuo vikuu inakidhi viwango vilivyowekwa.
Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Dk Leonard Akwilapo wakati akifungua kikao kazi cha wajumbe wa bodi wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu, Seneti na Bodi za Utawala za taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vishiriki.
“Nasisitiza taratibu zote zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa elimu ya juu ni lazima zifuatwe, hii inahusisha ufundishaji uliokamilika.
“Nafahamu tuna changamoto ya kuwa na wanafunzi wengi, hivyo ni lazima kuwe na mbinu mbadala kuwafanya wanafunzi wote wapate elimu inayostahili. Ndiyo maana nawataka msisitizo uwekwe kwenye ufundishaji, utahini na utoaji matokeo lazima viwe katika viwango vinavyokubalika,” amesema Dk Akwilapo.
Amesema bado taasisi za elimu ya juu zina jukumu la kuhakikisha vyuo vikuu vya Tanzania vinafika anga za kimataifa na kuongeza ushirikiano na vyuo vingine duniani.
“Tumefanikiwa kuwaandaa vijana ili wawe kimataifa lakini kuwa kimataifa inahusisha tafiti na mambo mengine ya kitaaluma. Tunataka tujiweke katika ngazi ambayo na sisi tutakubalika.
“Kufanikisha hilo ni lazima tunoane na kukumbushana umuhimu wa kufanya tafiti ambazo zitaleta masuluhisho kwenye changamoto zinazotukabili kwenye jamii yetu na hata zikawe na msaada hata kwa wenzetu wa mataifa mengine,” amesema.
Dk Akwilapo pia amezitaka taasisi za elimu ya juu nchini zimetakiwa kuoanisha programu zao na Sera ya Elimu na Mafunzo iliyorekebishwa na mtalaa wa Elimu ya Msingi na Mafunzo ya Ualimu ili kuendana na maboresho yanayoendelea kufanyika kwenye sekta ya elimu.
Amesema programu zote zinazotolewa katika taasisi za elimu ya juu zinapaswa kuoanisha na maboresho hayo yaliyofanywa na Serikali ili kukidhi matarajio ya wadau.
“Ninashukuru kwamba baadhi ya vyuo vikuu vimefanya maendeleo makubwa katika kuoanisha mtaala wao kama inavyotolewa na Tume kwa nyakati tofauti. Niombe taasisi zote za elimu ya juu tulitekeleze hili.
“Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 mtaala wa Elimu ya Msingi na Mafunzo ya Amali. Kupitia kikao hiki ni muhimu mkaangalia suala la kuoanisha programu za vyuo vikuu na Sera ya Elimu na Mafunzo iliyorekebishwa na mtaala wa Elimu ya Msingi na Mafunzo ya Ualimu.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema pamoja na mambo mengine wajumbe hao watajadili miongozo ya namna ya kupokea wanafunzi wa kimataifa kujiunga na vyuo vikuu nchini.
“Duniani mifumo ya elimu haifanani kwa kutambua hilo, TCU imetoa miongozo inayoeleza ni namna gani wanafunzi kutoka vyuo vingine duniani ambao mifumo yao ya elimu haiendani na yetu wanaweza kudahiliwa kwenye vyuo vyetu.
Hii ni katika juhudi ya kuhakikisha vyuo vyetu vinakuwa vya kimataifa, tumekuwa tukipokea wageni kutoka nchi mbalimbali duniani lakini sasa kwa miongozo hii ni imani yetu tutapata wanafunzi wengi zaidi wa kimataifa,” amesema Profesa Kihampa.