Lema awaomba radhi aliowakosea, waliofanya ‘vurugu’ kikaangoni

Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amewaomba radhi watu wote ambao amegombana nao katika kipindi cha uchaguzi wa chama hicho na kutaka waanze upya.

Aidha amekemea vurugu zilizojitokeza katika uchaguzi wa viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa wa Arusha akiwataka wanachama wa chama hicho kulinda nidhamu ya chama kwa wivu mkubwa.

Msingi wa kauli hiyo ni kile kilichotokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Novemba 14, 2024 kwenye uchaguzi wa chama hicho ambapo baadhi ya wanachama waling’aka na kumtuhumu Lema kuuvuruga uchaguzi huo.

Lema ameyasema hayo bada ya kumalizika kwa uchaguzi huo ambapo kabla ya kuhitimisha ilitokea hali ya sintofahamu baada ya baadhi ya wanachama kuanzisha vurugu huku wakidai uchaguzi huo umeghubikwa na rushwa.

Pia, makada hao walimtuhumu Lema kuwapambania baadhi ya wagombea akitaka washinde.

Katika maelezo yake baada ya uchaguzi kumalizika, Lema amesema, “Wote nyie mnafanya kazi kubwa sana, wale wote ambao mimi tumegombana kipindi hiki chote naomba mnisamehe sana, kabisa mnisamehe tuanze moja.”

 “Lakini wale ambao wamekuwa watovu wa nidhamu pale chini na sina uhakika kama huu ukumbi tutapewa tena, matusi yalikuwa mengi sana pale chini, udhalilishaji ulikuwa mkubwa,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema ni muhimu nidhamu kulindwa ndani ya chama na atakayekiuka achukuliwe hatua kuanzia ngazi ya wilaya hadi majimbo na kutokana na kazi hiyo kuwa ya kujitolea wana wajibu wa kujitolea kwa nidhamu.

“Ni bora tuwe na watu 10 wenye nidhamu kuliko watu 1,000 wasio na nidhamu, mkishindwa kulea nidhamu kwenye hiki chama, kitapotea kabisa,” amesema.

Mbunge huyo wa zamani wa Arusha Mjini ametolea mfano ukubwa wa vyama kama vya CUF, NCCR-Mageuzi chini ya uongozi wa Agustine Mrema (marehemu kwa sasa) na baadaye kuhamia TLP, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo ambapo amedai vyote vimepungua nguvu.

“CUF ilikuwa ni chama kikuu cha upinzani, NCCR mnakumbuka jamani, Lyatonga (Mrema) alikuwa akipita barabarani wamama wanatandika kanga majani na nini, TLP leo haipo kabisa, Cheyo wa UDP kuna kipindi Kanda ya Ziwa ukitaka kufanya ushirikiano wa kisiasa lazima umuone Cheyo,” amesema.

Lema amesema chama hicho kimejengwa kwa gharama kubwa na kimepitia misukosuko mingi ila bado kiko imara na kutokana na watu wengi kuwa na matumaini nacho lazima nidhamu idhibitiwe.

“Watu wana matumaini na hiki chama nyie, kizazi hiki angekuwepo bado mzungu bado tungetawaliwa,” amesema akiwapa ujumbe vijana wa chama hicho wa Bavicha kusimama imara.

“Bavicha ndiyo viongozi wa kesho, hapa katikati yenu kuna mbunge, waziri na mimi nawaambia usije ukatafuta suti kugombea ubunge, imani inaweza ikapanda mlima wowote ule,” amesema.

“Na udiwani kwenye kata hatutaangalia suti tutaangalia kamanda, tukiheshimiana, tutakisaidia chama kupata viongozi wazuri, mimi nikionaga Arusha inataka kuharibika nasikia vibaya maana tukiharibu Arusha tunaharibu Kaskazini,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure amesema wanachama hao walisoababisha vurugu hawakuwa wajumbe wa chaguzi hizo na kuwa  vikao vitafanyika kwa mujibu wa taratibu za chama hicho na kujadili suala hilo.

“Tutajadili haya mambo ya kutoa maelekezo ngazi za majimbo na wilaya na hatua za kinidhamu dhidi yao zitachukuliwa, wataitwa, watasikilizwa na kutolewa uamuzi kwani ukijaribu kuangalia kuna wengine wanatoka Kiliamanjaro, wanakuja kufanya fujo Arusha,” amesema.

“Wengine wanatengeneza timu na wengine wanajiandaa kutaka kuwa viongozi wa kanda, Chadema haya mambo kutokea hatuyapendi. Tutawaita, tuwasikilize na wakikutwa na hatia taratibu zitafuatwa ikiwemo adhabu, kuwaonya au kuwasimamisha,” amesema.

Related Posts