CCT yabainisha kasoro tano uchaguzi Serikali mitaa

Dar es Salaam. Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), imeainisha kasoro tano ilizozibaini katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kuanzia uandikishaji hadi ngazi ya uteuzi wa wagombea, huku ikisisitiza umuhimu wa uchaguzi huo kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Kasoro hizo ni malalamiko kuhusu daftari la wakazi, kuenguliwa wagombea, vikwazo katika kuchukua na kurejesha fomu, mapingamizi ya rufaa, kutekwa na kujeruhiwa kwa wananchi kunakohusishwa na masuala ya siasa na uchaguzi.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Novemba 14, 2024 na Mwenyekiti wa CCT, Askofu Fredrick Shoo alipotoa tamko la jumuiya hiyo baada ya kikao cha kamati ya utendaji kilichojadili mwenendo wa siasa nchini.

Kabla ya kueleza hayo mbele ya wanahabari, Dk Shoo amesema CCT imekuwa ikifuatilia kwa umakini mchakato wa uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kuanzia mwanzo, ikishiriki pia kutoa maoni wakati wa uandaaji wa kanuni zake.

“Kumekuwa na malalamiko kuhusu uandikishaji wa wapigakura wasiokuwa na sifa, ikiwamo kuwepo kwa majina ya watu waliofariki dunia,” amesema.

Ili kurekebisha karoso hizo, CCT imeitaka Wizara ya Tamisemi kufanya uhakiki wa daftari hilo kuhakikisha wananchi wote watakaopiga kura wanakuwa na sifa stahiki.

Amesema CCT imebaini uwepo wa malalamiko ya wagombea kuenguliwa kwa makosa madogo ikiwamo kushindwa kuandika majina matatu au anuani.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi, Novemba 12 alizungumzia kuhusu uchaguzi huo akiiomba Tamisemi kupuuza makosa madogo-madogo yaliyojitokeza wakati wagombea wakijaza fomu ili kuwepo wagombea wengi katika uchaguzi huo.

Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliongeza muda wa uwasilishaji rufaa hadi kesho Novemba 15, saa 12.00 jioni, akizitaka kamati za rufani za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa ili kufanya mapitio na kujiridhisha na sababu zilizosababisha wagombea kutoteuliwa ili haki itendeke kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi huo.

Askofu Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini amesema CCT imebaini baadhi ya wagombea wa upinzani waliwekewa vikwazo wakati wa urejeshaji fomu baada ya kukuta ofisi za watendaji zimefungwa.

Hata hivyo, Novemba 12, katika kikao na wahariri na wanahabari, Mchengerwa aliwahakikishia Watanzania kwamba hakuna mtendaji aliyefunga ofisi wakati wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo.

Mbali ya hayo, Dk Shoo amesema: “Tumeendelea kushuhudia kwa siku za hivi karibuni watu kupotea na wengine kuuawa tunapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa. CCT inakemea vitendo hivyo na kuzitaka mamlaka husika kufanya ufuatiliaji wa kina utakaohakikisha kupatikana kwa majibu ili kuondoa taharuki na hofu kwa jamii.”

Amesema CCT inasisitiza umuhimu wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kusimamia haki na usawa.

Hata hivyo, inapongeza mamlaka kwa jitihada za kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa uwazi.

“Tunasisitiza umuhimu wa chaguzi zote kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na marekebisho ya Katiba ili kuondoa changamoto zinazoathiri mchakato wa uchaguzi kila wakati nchi inapoingia katika chaguzi.

“Mwaka 2025 tutakuwa na uchaguzi mkuu, hivyo kama hatutachukua hatua stahiki tutakuwa na changamoto hizi-hizi. CCT tunavikumbusha vyombo vya dola hatutaki kuona yale yaliyotokea katika chaguzi wa 2019/20 yanajirudia tena mwaka huu. Watanzania wana haki ya kugombea na kuchagua viongozi wanaowataka bila shinikizo lolote,” amesema.

CCT pia imetoa wito kwa Watanzania kujitokeza kupiga kura, kufuatilia kampeni na kuchagua kwa hekima, kulinda amani na utulivu.

CCT imevitaka vyama vya siasa kusimamia vema kampeni za wagombea wao ili kuepuka lugha za matusi zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi. Pia, kuweka mawakala wenye weledi watakaosimamia vizuri mchakato wa kupiga kura, kuhesabu, kujumlisha hadi kutangaza matokeo.

Imewataka wasimamizi wa uchaguzi huo kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, usawa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa bila upendeleo wa aina yoyote.

“Tunatumia fursa hii kukemea na kuitaka wizara kuwachukulia hatua pale inapothibitika wasimamizi hawa wamefanya makusudi au kwa uzembe, hii itasaidia kurejesha amani kwa wananchi.

“Tunahimiza mamlaka husika kuzingatia usawa na uwazi katika kutangaza matokeo halisi ya uchaguzi kwa kuzingatia muda bila ucheleweshaji wowote ambao mara nyingi unasababisha kukosekana kwa imani kwa wananchi na matokeo husika,” amesema Dk Shoo.

CCT inaundwa na makanisa ya KKKT, Anglikana Tanzania, Morovian, Africa Inland Church of Tanzania, Kanisa la Mennonite Tanzania, Jeshi la Wokovu, Kanisa la Wabaptist Tanzania, Presbyterian Church of East Africa, Kanisa la Mungu Tanzania, Kanisa la Biblia Tanzania, Kanisa la Uinjilisti Tanzania na Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi.

Related Posts