Dar es Salaam. Ni kawaida kwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujitokeza hadharani kukanusha hoja zinazoibuliwa na makada wake.
Safari hii chama hicho kimeibuka kumjibu kada wake ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu, ikiwa ni baada ya siku 89 kupita tangu kilipomjibu juu ya madai ya rushwa ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, safari hii si Lissu pekee aliyejibiwa lakini hata aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa.
Miongoni mwa hoja zilizotolewa na Lissu na Dk Slaa kwa nyakati tofauti ni pamoja na ahadi ya kugawana madaraka na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Japo ufafanuzi uliotolewa na Chadema haukuwataja Lissu na Dk Slaa kwa majina lakini inafahamika Lissu ameibua hoja ya kugawana madaraka maarufu kwa jina la nusu mkate, huku Dk Slaa akihoji kwa nini chama hicho kimekaa kimya, wakati kiongozi wake (Lissu) akiibua tuhuma za rushwa.
Hatua hiyo imekuwa ikiibua mijadala ndani na nje ya chama hicho hasa ikizingatiwa Lissu kwa nafasi yake, ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama na ana uwezo wa kuzungumza kwenye vikao halali pasipo kutoka hadharani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus akizungumzia hali hiyo inayoweza kutafsirika kama mvutano, amesema ni dalili ya kutoelewana kati ya Lissu na baadhi ya viongozi wa chama hicho.
“Lissu hafurahii hali inayoendelea ndani ya Chadema na anaelekeza malalamiko yake kwa chama na viongozi. Akiwa miongoni mwa viongozi hao, kauli hizo zinaonyesha Lissu hakubaliani na hali inavyoendelea ndani ya chama chake na anatamani kungetokea mabadiliko lakini anaogopa kusema waziwazi,” amesema.
Dk Kristomus pia amesema Lissu hakukubaliana na uamuzi wa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kukaa meza moja na Rais Samia Suluhu Hassan kutafuta maridhiano.
Mhadhiri huyo amekumbushia makubaliano ya mwaka 2015 ya chama hicho na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiunga nao akitokea CCM.
“Nadhani anafahamu ushirikiano wa Mbowe na viongozi wa CCM umekigharimu zaidi chama chake kuliko kunufaika. Ikumbukwe makubaliano ya Mbowe na Lowassa mwaka 2015 yalikigharimu chama hata kama kilinufaika na idadi ya wabunge,” amesema.
Mwaka 2015, Lowassa ambaye alifariki dunia Februari 10, 2024, alihamia Chadema baada ya jina lake kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM. Chadema walimpitisha kuwania urais na alichangia kwa sehemu kubwa kuongeza idadi ya wabunge, madiwani na kura za urais.
Novemba 12, 2024 akizungumza na waandishi wa habari Singida Mjini, kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa serikali za mitaa, Lissu alisema chama hicho kilidanganywa wakati wa maridhiano na CCM.
“Tumedanganywa tukadanganyika, tumeletewa lugha laini ya uongo ya maridhiano. Tukaingiziwa vijineno vinavyosema hivi, msiwe wakali sana mtapewa Serikali ya nusu mkate.
Serikali ya umoja wa kitaifa, baadhi yenu mtakuwa mawaziri, wengine mawaziri wakuu labda, wengine makamu wa rais, wengine wabunge, mtapewa viti vya Bunge na CCM vya bure, msiwe wakali,” alisema Lissu.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Novemba 14, 2024 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, imesema Chadema haijawahi kuletewa hoja ya kugawana madaraka kutoka chama chochote au kutoka kwa Serikali wala hoja ya kupewa majimbo ya uchaguzi au kugawana nafasi za madaraka katika muundo wa Serikali.
“Chadema katika vikao vyake vyote rasmi haijawahi kujadili, kutoa au kupokea mapendekezo yoyote ya kitu kinachoitwa “Serikali ya nusu mkate”. Jambo hili kama linavyopotoshwa halijawahi kuwa sera ya Chadema.
“Ieleweke kwa mujibu wa Katiba iliyopo sasa nafasi ya Makamu wa Rais hugombewa na haitolewi mezani. Vilevile nafasi ya Waziri Mkuu hutokana na chama chenye wabunge wengi bungeni,” amesema Mrema.
Amesema vikao vyote vya maridhiano vilifanyika mwaka 2022 na vikahitimishwa Januari 3, 2023 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na Taifa kupitia vyama vya siasa na wadau mbalimbali, kuondoa katazo haramu la shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano.
“Mei 30 na 31, 2023 palifanyika vikao vya mwisho ambapo tulishindwana. Baada ya hapo hakuna kikao chochote cha siri au hadharani kimefanyika baina ya CCM na Chadema,” amesema.
Akizungumzia hoja ya chama kudanganywa na kuacha ajenda zake za msingi, Mrema amesema kwa kipindi chote cha mwaka 2023 na 2024 hadi sasa, chama hicho kimekuwa kwenye programu mbalimbali zenye lengo la kukiuhisha.
“Shughuli zilizofanyika ni pamoja na ziara mbalimbali maeneo kadhaa ya nchi kwa ajili ya mikutano ya hadhara, maandamano, mafunzo, usajili wa wanachama kidigitali, chaguzi kuanzia ngazi za vitongoji, mitaa, vijiji, kata, majimbo, wilaya, mikoa hadi kanda.
“Chaguzi hizi za ndani zitahitimishwa na uchaguzi mkuu ndani ya chama,” amesema.
Kuhusu tuhuma za rushwa, Mrema amesema zimekuwepo maeneo kadhaa, baadhi zimekosa vielelezo vya ushahidi wa kisheria na maeneo mengine bado uchunguzi wa ndani unaendelea.
Tuhuma hizo zimewahi kutolewa kwa nyakati tiofauti na Lissu, akidai kuingizwa kwa fedha ndani ya chama hicho kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi.
Lissu amerudia kauli hiyo jana Jumatano, Novemba 13, 2024 alipokuwa akihutubia mkutano wa uchaguzi wa chama hicho mkoani Singida.
“Kwenye uchaguzi mapesa yapo kila mahali. Naomba ujiulize, hayo mapesa ni ya kwetu kweli? Hiyo asali ni ya kwetu? Kama sio ya kwetu, jiulize ni ya nani na tunalambishwa kwa manufaa ya nani? Ukishajiuliza hivyo kapige kura.”
Tuhuma hizo alianza kuzitoa wakati wa uchaguzi wa kanda ya Nyasa uliokuwa na mvutano mkali hususan nafasi ya uenyekiti ambapo Joseph Mbilinyi maarufu Sugu alimbwaga aliyekuwa anatetea nafasi hiyo, Mchungaji Peter Msigwa.
Agosti 17, 2024 Chadema kilijitokeza hadharani na kujibu tuhuma hizo za rushwa na matumizi mabaya ya fedha, kikidai hakifahamu na aliyezitoa azithibitishe.
Hoja hiyo hizo za Lissu zimezungumzwa hivi karibuni na Dk Slaa kwenye mjadala wa mtandaoni ‘club house ya Sauti ya Watanzania! Akihoji sababau za chama hicho kukaa kimya baada ya Lissu kuibua hoja za rushwa ndani ya chama.
“Makamu Mwenyekiti alitoka hadharani akayatangaza, alipotangaza kwa nini hakitoki nje na kukemea? hawapaswi kuwachukulia wananchi kirahisi, wananchi wanahitaji heshima ya hali ya juu.
“Najua nachafua hali ya hewa, lakini niwe kwenye rekodi, nimesema yaliyoko moyoni mwangu kwa sabanu sipendi kubembelezana kwenye principles (misimamo).
Akijibu hoja hiyo, Mrema amesema Chadema imekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi, ubadhirifu na rushwa miaka yake yote.
“Kama chama kikiletewa ushahidi au vielelezo vya tuhuma hizo kutoka kwa mtu yeyote, tutafanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa katiba, kanuni na mwongozo wa chama dhidi ya rushwa wa mwaka 2012.
“Hivyo basi tunamwalika mtu yeyote mwenye ushahidi au vielelezo vinavyotosheleza kuwezesha kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahusika awasiliane na ofisi ya katibu mkuu au ofisi ya katibu yeyote wa kanda,” amesema.
Mrema amewataka wanachama wao na viongozi wote wa Chadema kuwekeza nguvu katika uchaguzi wa serikali za mitaa, na kupuuza propaganda za kukigawa chama.
Huko mkoani Arusha, hali ya sintofahamu imejitokeza katika uchaguzi wa viongozi wa Chadema, mkoa huo, baada ya baadhi ya wanachama wao kuleta vurugu wakituhumu uchaguzi huo kugubikwa na rushwa.
Wakizungumza usiku wa kuamkia leo Alhamisi Novemba 14, 2024, baadhi ya wanachama hao wamedai kufukuzwa kufuatilia uchaguzi huo na kuwa hawatakubali kuchaguliwa viongozi wasiowataka.
Akizungumza nje ya ukumbi ulikofanyika uchaguzi huo, mmoja wa wanachama wa Chadema Jimbo la Arusha, Boniface Kimario, alidai kuwa uchaguzi huo umeghubikwa ya rushwa.
“Wanatuharibia hiki chama…’’ amedai.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Alhamisi Novemba 14, 2024, Mwenyekiti wa kanda ya Kaskazini, Godbless Lema alisema angelizungumzia suala hilo kwenye uchaguzi wa viongozi Mkoa wa Manyara unaofanyika wilayani Babati.
“Unaweza ukatuma mwandishi wenu niko njiani ninakwenda Manyara kwenye uchaguzi nitatoa statement (taarifa) kwenye hotuba ya ufunguzi,” amesema. Hata hivyo, kwenye mkutano huo alioahidi kuzungumzia hakugusia suala hilo. Alipotafutwa tena hakupatikana.
Uchaguzi huo wa Arusha ulisimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, aliyekuwa akisaidiwa na Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa.
Akizungumzia tukio hilo, Golugwa amedai kuna watu wasiohusika ambao hawakuwa wajumbe hivyo hawawezi kuingia kwenye uchaguzi, kwani kanuni zinataka wajumbe peke yao.
“Kuna watu kwa sababu ambazo hatukuwa tumezielewa waling’ang’ania kutaka kuingia kwenye uchaguzi. Kwa mfano, uchaguzi wa wanawake wanaingia wanawake peke yao; kuna baadhi ya wanaume walitaka kuingia kwenye uchaguzi wa wanawake pia kuna watu ambao kwenye mchujo walikatwa, kwa sababu za kikanuni baadhi yao waliendelea kubeba hisia kwamba wanaonewa,” amesema Golugwa.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.
Nyongeza na Janeth Mushi.