SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limeifungia Klabu maarufu ya Morocco, Wydad Casablanca, kufanya usajili wa wachezaji kutokana na kushindwa kutekeleza malipo ya kifedha wanayodaiwa na mchezaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ambaye kwa sasa anaitumikia Al-Talaba SC ya Iraq.
Adhabu hiyo ni sawa na iliyoikumba mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara waliofungiwa kusajili kutokana na kushindwa kumlipa aliyekuwa mchezaji wao, Augustine Okrah anayewadai zaidi ya Sh60 milioni.
Msuva aliishtaki klabu hiyo FIFA kutokana na kushindwa kumlipa pesa za usajili sambamba na malimbikizo ya mshahara, Dola 700,000 (zaidi ya Sh1.6 bilioni).
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Mkuu wa Kamati ya Maadili ya FIFA, Americo Espallargas, Wydad haijatekeleza agizo la kulipa haki za kifedha zinazodaiwa na Msuva, jambo lililolazimu Fifa kuchukua hatua kali ya kuifungia klabu hiyo usajili wa kimataifa hadi pale watakapolipa deni hilo lote.
Hatua hii ina maana Wydad haitaruhusiwa kusajili wachezaji wapya kwenye mashindano ya kimataifa hadi malipo hayo yatakapokamilika.
Pia, Fifa imeagiza Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) kuhakikisha marufuku hiyo inatekelezwa pia kwenye mashindano ya ndani ya Morocco, ikiwa bado hawajachukua hatua hiyo.
Hii inaweka presha zaidi kwa Wydad kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa mchezaji huyo ili waweze kurejea kwenye hali ya kawaida ya usajili.
FIfa inasisitiza umuhimu wa kuheshimu mikataba na malipo ya wachezaji, ikionyesha dhamira ya shirikisho hilo kulinda haki za wachezaji na kuhakikisha klabu zinajali masuala ya kifedha katika uendeshaji wao.
Julai, 2022, Msuva aliishtaki Wydad kwa kosa la kuvunja mkataba kinyume na utaratibu baada ya kuwa katika mvutano wa kimaslahi na waajiri wake hao wa zamani ambao walimsajili Novemba 2020 akitokea Difaa El Jadida ya hapohapo Morocco.