Zayd ampa tabasamu Kocha Azam

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Rachid Taouss amefurahia kurudi kwa mastaa wake waliokuwa majeruhi huku akimtaja Yahya Zayd ni mchezaji ambaye anaweza kuziba mapengo mengi.

Nyota waliokuwa nje kikosini hapo na wamerejea baada ya kupona majeraha ni pamoja na Zayd, Yanick Bangala, Abdallah Heri ‘Sebo’ na Sospeter Bajana ambao wote wamerudi na wanaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Novemba 23 mwaka huu, Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Taouss alisema ni nzuri kwake kuwa na wachezaji wote kwenye maandalizi, hivyo anafurahia kurudi kwa wachezaji hao na kumtaja Zayd amemuonyesha anaweza kuziba mapengo ya wachezaji wengi.

“Niliambiwa ni kiraka ana uwezo wa kucheza maeneo mengi, nimejiridhisha kwenye uwanja wa mazoezi baada ya kumtumia katika maeneo ambayo wachezaji ninaowatumia wapo timu ya taifa,” alisema na kuongeza.

“Kuwa na mchezaji aina ya Zayd kikosini ni faida kubwa kwa sababu anakufaa kwenye nyakati zote pindi timu ikiwa na wachezaji wengi majeruhi anaziba nafasi zao ingawa sio zote lakini unampanga eneo ambalo unajua atakupa kitu unachohitaji.”

Kocha huyo raia wa Morocco alisema mbali na mchezaji huyo, pia wachezaji wengine wataongeza changamoto ya ubora kutokana na wingi wao kwenye nafasi moja.

“Wachezaji wote ni wazuri, kila mmoja anapambana kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza hawezi kufanya makosa kwa sababu anajua kuna mtu anamsubiri ili naye apate nafasi ya kuonyesha,” alisema na kuongeza.

“Ubora wa kikosi changu utategemea na kujituma kwa wachezaji wangu ambao kila mmoja anatamani kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ambacho kinahitaji ubora mkubwa kutokana na ushindani ulivyo kwenye Ligi.”

Related Posts