Dk. Ndumaro amualika Waziri wa michezo Ivory Coast kushuhudia ‘Derby’

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro, amemualika Waziri wa Michezo wa Ivory Coast Adjé Silas kushuhudia mechi ya Simba na Yanga ‘Derby ya Kariakoo’.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pili unatarajiwa kupigwa kesho Aprili 20, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam,

Ndumbaro amempa mualiko waziri huyo ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi  wakati walipokutana kufanya mazungumzo jijini Dar es Salaam.

Ndumbaro amesema amemualika ili aone ladha ya mechi hiyo kubwa Afrika Mashariki pamoja na kuwaona wachezaji nyota wa timu hizo akiwemo mchezaji Pacome Zouzoua wa Yanga ambaye ni raia wa Ivory Coast.

Mawaziri hao wawili  waliokutana kwa lengo la kufanya mazungumzo, wamejadili  juu ya ushirikiano wa nchi hizo kwenye sekta ya michezo.

Silas yupo nchini kwa ziara ya kikazi ambapo pia atashiriki hafla ya kuingia makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Ivory Coast katika sekta ya michezo itakayofanyika Aprili 21, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Related Posts