Mambo matano yanayoharibu ubongo wa mtoto

Dar es Salaam. Afya bora kwa mtoto inachangiwa na mambo mengi, ikiwamo chakula bora, usafi wa mwili na mazingira anayoishi. Vyote hivyo ni msingi mzuri wa hatua ya makuzi ya mtoto.

Hata hivyo, kuna makosa ambayo baadhi ya wazazi au walezi huchangia kwa kiwango kikubwa kuyumbisha hatua za ukuaji wa mtoto.

Makosa hayo mzazi huyafanya ama kwa kujua au kutojua na hujikuta akimuweka mtoto katika hatari ya kupata changamoto mbalimbali za kimwili na kiakili.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa masuala ya watoto kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Maria Bulimba anasema mambo hayo ambayo hufanywa na baadhi ya wazazi yana athari katika ustawi wa mtoto kimwili na kiakili.

Dk Bulimba anasema miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuruhusu watoto kutumia muda mrefu kutizama televisheni, simu au kompyuta mpakato kwa muda mrefu.

Anasema jambo hilo linaweza kuonekana ni la kawaida, lakini lina athari katika ukuaji wa mtoto, hasa likifanyika bila kipimo au kutozingatia miongozo.

Anabainisha kuwa kitaalamu na kwa mujibu wa miongozo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), mtoto wa chini ya miaka miwili haruhusiwi kabisa kuangalia televisheni au kutumia vifaa kama vile kompyuta mpakato, vishkwambi, simu ya mkononi pamoja na vinginevyo.

“Pia hata kwa yule aliye na umri wa miaka miwili na kuendelea, miongozo inaainisha ni kwa muda gani anaruhusiwa kutumia vifaa hivyo,” anasema.

Anaeleza kuwa kwa mtoto mwenye umri wa miaka miwili hadi mitano anaruhusiwa kuangalia televisheni au kutumia vifaa hivyo vya kidijitali kwa muda wa saa moja pekee.

“Kuanzia miaka mitano na kuendelea muda wa mtoto kutumia vifaa hivyo unaweza kuongezwa taratibu kadiri anavyozidi kukua, lakini kabla ya kufikisha miaka 18 mtoto hatakiwi kutumia vifaa hivyo kwa zaidi ya saa tatu,” anasema.

Hata hivyo, anaeleza kuwa wazazi wengi hawana uelewa juu ya hatari ya kuwaacha watoto kutumia muda mrefu vifaa hivyo na hivyo kuwaacha wakitumia bila ya uangalizi wa muda na hatimaye kuwaweka katika hatari ya kupata changamoto mbalimbali za kiafya.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kupata maumivu ya kichwa, kuumwa macho pamoja na kutopata usingizi wa kutosha, kutokana na kutumia muda mwingi kuangalia vifaa hivyo.

Ningeshauri sana hivi vifaa visitumike kwao, mara nyingi wazazi wana tabia mtoto akisumbua anampa simu, hususan kwa watoto wa chini ya miaka miwili, ile miale inaathiri macho yao mapema sana.

“Baadaye itakuja kumletea matatizo makubwa, ingawaje inachukuliwa kawaida lakini kila wakati ambao mtoto anashika ile simu anazidi kuyaangamiza macho yake,” anasema.

Daktari bingwa wa Fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Fredrick Mashili anaeleza kuwa mtoto kuangalia televisheni au vifaa hivyo vya kidijitali kwa muda mrefu kunaweza kumnyima fursa ya kuchangamana na watoto wenzake.

Anasema moja ya athari kubwa ni kupungua kwa shughuli za kimwili, watoto wanapokuwa mbele ya televisheni kwa masaa mengi, wanapoteza muda wa kucheza au kufanya mazoezi ya mwili.

“Hii inaweza kuongeza hatari ya kupata matatizo kama vile uzito kupita kiasi, ambayo ni tatizo linalozidi kuwa kubwa duniani,” anaeleza.

Vilevile Dk Mashili anagusia suala la wazazi kutozingatia lishe bora kwa watoto linavyowaweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza pamoja na uzito mkubwa wakiwa katika umri mdogo.

Pia anasema vinywaji vilivyoongezwa sukari haviruhusiwi kupewa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na vijana balehe chini ya miaka 19 kwa sababu za kiafya.

“Sio vinywaji vya viwandani peke yake, hata vinywaji vilivyotengezwa na kuongezwa sukari mtoto hapaswi kupewa,” anasema.

Pia anasisitiza chakula chenye mafuta mengi si sahihi, kwani ni hatari kiafya kwa mtoto na kuhimiza wazazi kuhakikisha wanakuwa makini kwa kile wanachowalisha watoto wao.

“Lishe bora ni muhimu sana katika ukuaji na maendeleo ya watoto. Ulaji usio sahihi una madhara makubwa kwa afya ya mtoto na kusababisha magonjwa mbalimbali,” anasema.

Kwa upande wake, Ofisa Mkunga Msaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga anasema kosa jingine wanalolifanya wazazi ni kuwafungia watoto sana ndani hadi kukosa fursa ya kuchangamana na wenzao.

Mganga anasema hili linamnyima mtoto fursa ya kuchangamsha ubongo wake na kujifunza vitu vilivyopo katika mazingira.

Anaeleza kuwa kwa mtoto wa chini ya miaka miwili huweza kumuweka katika hatari ya kuchelewa kuzungumza.

Anaongeza kuwa mtoto ambaye anapata fursa ya kucheza na watoto wenzake ni rahisi kujifunza lugha, hivyo kama hana changamoto zingine ana nafasi kubwa ya kuwahi kuanza kuongea kuliko yule ambaye anafungiwa ndani.

“Kama mtoto mdogo hachezi na watoto wenzake yeye ni amefungiwa ndani tu hakuna wa kuongea naye mara kwa mara, muda wake mwingi anaangalia tu televisheni au kuchezea simu akiwa katika umri mdogo, inaweza kumfanya kuchelewa kuongea,” anasema.

Anasema mtoto anapocheza na wenzie huwa ni njia mojawapo ambayo hujifunza maneno mapya, huyabeba na kuyatumia kila siku.

Related Posts