Namna ya kumsaidia kijana balehe kushinda hisia

Dar es Salaam. Kipindi cha mpito cha ukuaji kutoka utoto kuelekea utu uzima, hutafsiriwa kama rika balehe. Huu ni muda ambao mhusika siyo mtoto wala mtu mzima kibiolojia, wala hajakomaa kihisia.

Katika kipindi hiki yapo mabadiliko makubwa ya kimwili yanayohusiana na mwanzo wa kubalehe pamoja na kukua kisaikolojia.

Kijana balehe hujumuisha wanafunzi wengi walio kwenye shule za msingi na baadaye kukamilika wakiwa shule za sekondari.

Miongoni mwa changamoto zinazowakabili vijana hawa ni kukosa taarifa sahihi za masuala ya afya ya uzazi.

Katika kutanzua changamoto hizo, vijana wa rika balehe wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kukabiliana na mabadiliko ya kimwili na kihisia wanayoyapitia.

Mabadiliko hayo ni matamanio ya mwili, tatizo la lishe, changamoto ya afya ya akili, upungufu wa damu, uzito mkubwa na mdogo na ukosefu wa vitamini.

Wakati kijana anabalehe na kuanza kukumbana na changamoto za kihisia na matamanio ya kimwili, anakutana na familia ambayo wazazi au walezi wanashindwa kuvunja milango ya aibu na kuondoa tamaduni na vizuizi vya kijamii.

Swali linalogonga vichwani mwa wazazi na walezi wengi, ni upi wakati sahihi kuzungumza na mvulana au msichana anayebalehe kuhusu namna ya kuzishinda hisia zake.

Mhamasishaji Roland Malaba, maarufu kama Madenge anasema ni muhimu mtoto akaanza kuelekezwa kuhusu mwili wake na namna ya kujilinda angali mdogo na si kusubiri mpaka awe mtu mzima.

“Naanza kuongea na mwanangu toka anapozaliwa, inategemea tunazungumza nini. Ni kama ngazi, kadiri muda unavyoenda mazungumzo yangu na yeye yanabadilika, kufuatana na tabia zake naona huyu inabidi nianze kuzungumza naye, mazingira yanaamua uzungumze nini na mtoto, huenda umri unaoutaka wewe yeye akaanza mapema,” anasema.

Madenge, ambaye pia ni mtangazaji wa kipindi cha Joto la asubuhi EFM, anasema tatizo linazidi kuwa kubwa kwa sababu vijana wengi wanakosa taarifa, huku wazazi na walezi wakisubiri wafikishe miaka 18.

“Ukianza naye mapema ni rahisi kuja kuisimamia juu, mzazi unataka umpe taarifa miaka 18 kwa sababu ya kuogopa katikati ukimpa taarifa zinamshawishi yeye kufanya ngono, hapana, ni jinsi gani unatoa taarifa, ni namna ya uwasilishaji,” anasema.

Anasema mtoto hupokea kulingana na anavyoelekezwa. “Wenzetu Wazaramo wana tamaduni nzuri za kumcheza ngoma, lengo lilikuwa zuri, lakini namna mtoto anavyofanyiwa siyo, zipo taarifa anafundishwa kumridhisha mwanamume badala ya kujilinda na hii inakuja sababu tuna mkanganyiko wa kiimani na wa kimakabila.”

Madenge anasema kuna mwingiliano wa kidini, tamaduni za watu na kuna serikali na huko kote wanaongea lugha tatu tofauti.

Wadau mbalimbali wametaja umuhimu wa mzazi kuzungumza na kijana wake, ili kuzuia masuluhisho yao hasi katika kuzishinda tamaa za kimwili, zenye matokeo mabaya, ikiwemo kupata magonjwa na mimba za utotoni.

Mratibu wa kuzuia na kupinga ukatili wa kijinsia wa Shirika la Norwegian Church Aid, Zaria Mwenge katika mkutano ulioandaliwa na Mtandao wa Taasisi za Kitaifa za haki za Binadamu Afrika (NANHRI) anasema ngono isiyo salama ni changamoto kwa vijana balehe.

“Wakati mwingine wamekuwa wakifanya ngono na wanyama na hii tumepata kutoka kwa vijana wenyewe, ukienda katika jamii ya wafugaji mkoani Manyara kwa mara ya kwanza wanapoanza ngono hufanya na wanyama,” anasema.

Aina ya wanyama aliowataja vijana hao kushiriki nao ngono ni ngombe, punda, kuku pamoja na paka, huku ndugu wa karibu baba na mwanaye, kaka na dada nao wakishiriki tendo hilo kwa siri.

Zaria anasema tatizo lipo kutokana na vijana hao kukosa taarifa sahihi ya masuala ya afya ya uzazi kutokana na jamii kutoruhusu vijana ambao hawajaingia kwenye ndoa kuzungumzia masuala ya uzazi.

“Kwa sababu wakati huo wanashawishika kufanya hivyo, wanatumia njia za siri, ikiwemo kufanya ngono na wanyama, pia utakuta kijana anafanya ngono na dada yake, mama ana uhusiano na kijana mdogo, haya ni mambo yanayoendelea kwenye jamii yetu,” anasema.

Anasema matukio hayo hufanyika kwa siri na ndio huwa chanzo ya changamoto ya afya ya akili kwa vijana, huku wasichana wakizishinda hisia kwa kuweka ugoro sehemu za siri.

“Wasichana wanakuambia wanatumia ugoro kama njia ya kumaliza haja zao za kimwili, huyu anaingiza ugoro sehemu za siri na huku tunapambana na saratani, hili ni tatizo, tunachopaswa kufanya ipo miongozo mingi inayohusu vijana, ni muhimu miongozo hiyo ikashuka chini, watu wapewe elimu mwongozo unasemaje na unataka matokeo gani,” anasema.

Pia anashauri viongozi wanaopewa mamlaka ya kuongoza kundi la vijana, wawe na elimu sahihi kuhusu kundi hilo ili kuwe na matokeo chanya katika utendaji wao.

Jambo lingine analopendekeza Zaria ni kijana kupewa elimu kuhusu mabadiliko ya mwili wake, jukumu hilo akiwatwisha wazazi na walezi.

Anasema vijana wanapopewa elimu na wazazi na walezi kuhusu mabadiliko ya miili yao, itawasaidia mabadiliko yoyote wanayoyaona kuwapa taarifa.

“Kinachotuumiza sasa jukumu la malezi kaachiwa mama peke yake, yapo mazungumzo ya mtoto wa kiume mama hayamhusu kwa sababu siyo mwanamume. Baba ana uwezo wa kuzungumza na kijana wake kwa sababu amepitia hizo changamoto, kama wazazi wataamua kutulia watoto watajifunza kwa wenzao au kwenye mitandao,” anasema.

Kwa upande wake mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha, anasema watoto kuanzia miaka mitatu wanafahamu mambo mengi kuliko watu wazima.

“Bila kuwa na kiongozi hatuwezi kufanya kitu, kila mtu atajichukulia maamuzi, tunahitaji uratibu makini, ukisikia Wizara ya Elimu wana mipango yao, Wizara ya Afya ina mambo yao, sasa tunapokuwa kwenye vikao vya kuweka vipaumbele vya taifa lazima tutenge bajeti inayomgusa kijana na mtoto kwa kutambua makundi haya ni mbegu ya baadaye,” anasema.

Kuhusu eneo la lishe, Eveline Maziku kutoka Wizara ya Afya Idara ya Uzazi, Mama na Mtoto anasema changamoto inayowakumba vijana balehe ni kutozingatia lishe bora.

“Vijana vyuoni wanakiri wanakunywa ‘energy’ asubuhi, anabaki hana njaa kuanzia muda huo hadi jioni akila, hadi kesho tena, hiyo fedha wanabana ili wakanunue simu mpya, Serikali inaendelea na jitihada za kuhamasisha lishe bora,” anasema.

Anasema kwa mwaka 2022 maambukizi mapya ya Ukimwi yalikuwa 60,000 na kupitia takwimu hiyo vijana balehe walikuwa robo tatu.

Yoyce Barahuga kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia masuala ya uzazi salama, anasema vijana wa umri balehe kuanzia miaka 15 hadi 19 katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari ni maeneo wanayoangalia kwa umakini.

Anasema kwa shule za sekondari wapo walimu wa malezi na afya, msisitizo wao mkubwa ni vijana kupewa elimu ya usafi kujiepusha na magonjwa mbalimbali.

“Kitu kingine ni kuelezwa kuhusu hatua zao za ukuaji, ulinzi dhidi ya magonjwa ili wawe salama pamoja na kufundishwa namna maumbile yao yanavyobadilika,” anasema.

Kitu kingine anachoeleza Joyce ni maadili kwa wanafunzi na ulaji wa mlo bora kuepukana na ushawishi wa wasichana kulaghaiwa na madereva bodaboda na watu wengine wasio na maadili.

Kwa upande wake, Gladness Kirei wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anasema wizara hiyo imeandaa miongozo mbalimbali, ikiwemo unaohusu stadi za maisha, ukilenga elimu ya afya ya uzazi, Ukimwi na jinsia.

“Walimu zaidi ya 5,533 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kusaidia vijana, tunaendelea kusambaza miongozo na kutoa elimu kwa walimu namna ya kuwasaidia vijana kwenye masuala ya afya ya uzazi,” anasema.

Kirei anasema tayari mwongozo wa urejeshwaji wanafunzi shule waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali umeendelea kutekelezwa na zaidi ya wanafunzi 22,000 wamerejea masomoni, wengi wao waliopata ujauzito.

Related Posts