Gamondi, uongozi Yanga changamoto ni hii

VICHAPO mara mbili mfululizo ilivyopata Yanga vimeibua mambo mengi kwa taswira ya ndani ya timu hiyo kujionyesha dhahiri ambapo hatua ya kwanza ya mabosi wa timu ni kwamba wanajipanga kumpiga chini kocha wao Miguel Gamondi.

Yanga inaona msalaba wa kwanza anayepaswa kubebeshwa ni kocha wao Miguel Gamondi ambaye anaonekana kama falsafa zake zimeshakuwa kitu rahisi kukamatika kwa wapinzani wao.

Makosa ya kiufundi ambayo kocha huyo ameyaonyesha yakiwemo namna ambavyo ameshindwa kutengeneza timu inayolingana kiushindani baina ya wachezaji, ni kati ya mambo yanayomfanya Gamondi kujikuta amekalia kiti cha moto.

Ukitazama namna mtangulizi wake Nasreddine Nabi alifanikiwa kutengeneza kikosi kilichokuwa na ushindani sahihi wa nafasi za wachezaji, ilikuwa ngumu kuona tofauti kubwa anapocheza Kibwana Shomari dhidi ya Djuma Shaban, au hata anapocheza Zawadi Mauya au Khalid Aucho.

Hili limeshindwa kuwa endelevu kwa Gamondi ambaye ni kama alikuwa na kundi moja tu la wachezaji anaowaamini ambao nje yao inaonekana ni ngumu kupenya na kuisaidia tena timu hiyo. Hata hivyo, yapo mambo mengi ambayo mabosi wa Yanga wanatakiwa kuyafanyia kazi hata kama wataafikiana kumuondoa kocha huyo ambapo kama hawatayafanyia kazi inaweza kuendelea kuwasumbua.

Endapo Yanga itamuondoa Gamondi inahitaji kocha mwenye ubora mkubwa ambaye atakuja kuiunganisha timu hiyo kwa haraka, ambaye anajua namna ya kushinda dhidi ya wapinzani wao kwenye mechi za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo ajue namna ya kuishi na wachezaji wakubwa ambao hapa ndani tunaamini wana majina makubwa lakini kikubwa lazima awe na msuli wa kusimamia nidhamu mbele ya wachezaji wake.

Sio jambo la kujificha kwamba nidhamu kwa baadhi ya wachezaji wa Yanga imeshuka, hata uwe na msuli gani wa utetezi huwezi kupinga namna wachezaji wa Yanga wanavyozagaa wakifanya starehe hatarishi ndani ya msimu.

Mbaya zaidi wachezaji hao wameshindwa kutunza hadhi yao kwa kujiachia wakirekodiwa na kwa nyakati kama hizi video za namna hiyo hata kama starehe hizo zitakuwa zilifanyika katika nyakati zilizostahili, hakuna ambaye anaweza kuwaelewa.

Kama kuna kocha anayekuja, basi lazima akubali yaishe. Yaani hata kama atakuja na kiwango gani cha uelewa na weledi, itabidi asome alama za nyakati. Kwa sasa muda wa kukaa kambini Yanga umepungua, jambo hili kwa soka la Bongo ni tatizo kubwa. Gamondi alikuwa anaiingiza timu yake kambini siku moja kabla ya mchezo yaani Yanga iliingia kambini Jumatano kisha ikaenda kucheza na Tabora United Alhamisi, ikitokea wachezaji wakashindwa kujilinda sawasawa huko mtaani ni vigumu kocha kueleweka.

Achana na kikosi cha Yanga, angalia mashabiki wao na hata baadhi ya viongozi baadhi yao walionyesha kama timu yao ni vigumu kufungika tena, hali ilikuwa kama wameshindikana, wakajisahau kwamba kuna timu zinaumiza vichwa kwamba watawezaje kuwazuia.

Ndani ya Yanga kuanzia mashabiki, viongozi mpaka wachezaji wanatakiwa kubadilika wakitambua kwamba hata uwe bora namna gani, unaweza kufungika kama utashindwa kutunza ubora wako kwa kuridhika.

Wengi ndani ya Yanga wakiona kikosini wana watu kama Clatous Chama, Pacome Zouzoua, kule Stephanie Aziz KI mara huku yupo Ibrahim Bacca basi kazi imekwisha, wanasahau kwamba ndege mjanja hunaswa tundu bovu.

Wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuambiwa ukweli zaidi na zaidi kwamba majina yao hayatashinda mechi bali kwa kuzingatia nidhamu ya mchezo na pia kwamba viongozi wa klabu hiyo walisajili vipaji vyao na sio ukubwa wa majina yao.

Kubomoka kwa nidhamu ya wachezaji wa Yanga, wengi watawalaumu nyota wao, lakini kuna hawa wapambe ambao sasa wanaitwa ‘chawa’. Uongozi wa klabu hiyo ni lazima uwatazame chawa hawa kwa jicho la ukali kwani wana ushawishi mbaya kwa wachezaji.

Ukizunguka usiku unakutana nao wako na wachezaji wao, kukicha utawaona wako na viongozi wao, likishaibuka balaa kama hili haraka wanakaa upande wa viongozi.

Kundi hili ni hatarishi zaidi, linajua kuunganisha watu na kisha kukaa pembeni wanasubiri anguko ili kisha wauwashe moto. Nani anatakiwa kuokoa jahazi ni viongozi wenyewe kwa kuwaambia ukweli wachezaji wao kwamba wanaokaa nao na kufanya nao starehe ndio haohao watasambaza mambo yao endapo watakosa kujitambua kufanya mambo yao bila ya weledi.

Ni ngumu kudhani kama kuna shabiki wa Yanga alifikiria kwamba nyakati kama hizi anayeongoza kwa ufungaji angeweza kuwa mshambuliaji Seleman Mwalimu wa Fountain Gate au watani wao Simba watakuwa juu ya msimamo au hata kikosi chao kingepoteza kwa timu kama Tabora United tena kwa mabao 3-1.

Yanga wanatakiwa kutambua ligi ni ngumu na kila timu inautaka ubingwa, watani wao wamebadilika, wamefanya usajili mkubwa na kiufupi kila timu imejipanga kwa hesabu zake, hivyo haitakuwa rahisi kwao kutetea ubingwa endapo wataendelea kujiona kama wao ndio bora kuliko wengine.

Related Posts