Makundi haya yanaongeza ushamiri wa VVU

Dodoma. Makundi ya madereva wa masafa marefu, wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi na vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 yametajwa kuwa bado yana ongezeko la ushamiri wa Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa viashiria vya Ukimwi mwaka 2022/23, idadi ya watu wanaoishi na VVU nchini imepungua kutoka milioni 1.7 mwaka 2016/17 hadi milioni 1.5 mwaka 2022/23.

Utafiti huo unaonyesha kuwa ushamiri wa VVU kitaifa ni asilimia 4.4 ikilinganishwa na asilimia 4.7 kwa mwaka 2016/17.

Akizungumza Novemba 14, 2024, kuelekea Siku ya Ukimwi Duniani, Desemba mosi, 2024, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Jerome Kamwela amesema wamepanga mikakati kulingana na aina ya kundi kwa kuhakikisha huduma zinawafikia kwa urahisi.

“Kwa vijana wa miaka 15 hadi 24 wanachangia theluthi moja ya maambukizi mapya ya VVU, kwa hiyo tuna miradi ambayo inawalenga vijana, mfano wa  ule wa wasichana balehe na wanawake vijana unaoendelea katika mikoa 10 nchini,” amesema.

Amesema pia wana miradi ya kuhakikisha huduma zinafika kwa wavuvi pamoja na vituo vya huduma pembezoni mwa barabara kuu, kwa madereva wanaokwenda masafa marefu.

Awali akizungumza kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado kumekuwa na kuongezeka kwa ushamiri miongoni mwa baadhi ya makundi hayo.

“Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua fursa hii kuendelea kuwasihi wananchi wote kujikinga na kutumia dawa kwa usahihi kwa wale waliojitambua wanaishi na maambukizi ya VVU,” amesema.

Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Ummy amesema maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika mkoani Ruvuma ambapo siku ya kilele Desemba mosi, mgeni rasmi atakuwa ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

“Maadhimisho ya siku ya Ukimwi kwa mwaka huu ni wito wa kulinda afya ya watu wote kwa kuchagua njia sahihi ili kutokomeza Ukimwi,” amesema.

Amesema maadhimisho hayo kutakuwa na huduma ya upimaji wa hiari wa VVU kwa wiki nzima kuanzia Novemba 24, 2024 hadi Desemba 1, 2024 siku ya kilele.

Pia katika maadhimisho hayo amesema kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo midahalo kwa vijana, viongozi wa kidini na wa kimila pamoja na kongamano la kitaifa la kisayansi kwa ajili ya kujadili mwitikio wa Taifa wa Ukimwi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na udhibiti wa Ukimwi suniani (UNAIDS), Dk Martin Odiit amefafanua kuwa kaulimbiu ya maadhimisho hayo imejikita kueleza kuwa dunia inaweza kumaliza Ukimwi kama kila haki ya mtu italindwa.

“Naipongeza Serikali kwa utashi wa hali ya juu waliouonyesha katika taarifa ambazo kila wakati anahamasisha umuhimu wa kumaliza Ukimwi,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Mchungaji Emmanuel Msinga ametoa wito kwa Watanzania kuchagua njia zilizo sahihi za kujikinga na VVU, kupima mapema, kuanza tiba ya Dawa za Kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARVs) na kuwa wafuasi wazuri wao na familia zao.

Related Posts