Yanga yaachana na Gamondi, msaidizi wake Moussa Ndaw

Klabu ya Yanga imemfuta kazi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi leo Ijumaa Novemba 15, 2024. 

Taarifa ya kufutwa kazi kwa makocha hao imetolewa na Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Yanga ikisema: “Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutarifu umma kuwa umevunja mkataba na Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, Angel Miguel Gamondi.

“Vilevile, Uongozi wa Young Africans Sports Club, umesitisha mkataba wa kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza, Moussa Ndaw.”

Aidha, taarifa hiyo imesema uongozi wa Young Africans Sports Club unawashukuru makocha hao kwa mchango wao ndani ya Klabu yetu na unawatakia kila la kheri katika majukumu yao mapya.

“Tayari mchakato wa haraka wa kutafuta Makocha wapya wa kikosi chetu cha kwanza umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde,”imeongeza taarifa hiyo.

AONDOKA NA REKODI ZAKE YANGA

Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mchezo huo wa fainali, Yanga ilichapwa jijini Dar es Salaam mabao 2-1 na USM Algers Mei 28, 2023, kisha marudiano ikashinda kwa 1-0, Juni 3, 2023 na Waalgeria hao kuchukua ubingwa huo kutokana na kufaidika na faida ya bao la ugenini.

Licha ya viongozi wa Yanga kujifungia kwa ajili ya kujadili mwenendo wa timu hiyo kutokana na kiwango ambacho Gamondi amekionyesha hadi sasa msimu huu, ila Mwanaspoti linakuletea rekodi tamu ambazo kocha huyo hata akiondoka atakumbukwa.

Tangu ateuliwe kukiongoza kikosi hicho, Gamondi amekiongoza katika jumla ya michezo 40 ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi huu wa sasa wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hiyo ameshinda 34, sare minne na kupoteza pia minne.

Katika michezo hiyo 40 ya msimu uliopita na huu wa sasa, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Gamondi imefunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu miwili amekusanya pointi zake 104.

Gamondi amechukua mataji matatu na timu hiyo akianza na Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kukifanya kikosi hicho kufikisha jumla ya mataji 30, tangu mwaka 1965, akachukua pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii kwa msimu huu.

Gamondi aliipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25, kufuatia kufanya hivyo mara ya mwisho 1998 wakati huo ikinolewa na kocha wa muda, Tito Mwaluvanda aliyempokea Mwingereza, Steve McLennan.

Mwaluvanda alipewa timu hiyo akiwa hana umaarufu wowote na aliyekuwa Mwenyekiti, Rashid Ngozoma Matunda ambapo kikosi hicho kiliangukia kundi la kifo na ASEC Mimosas (Ivory Coast), Manning Rangers (Afrika Kusini) na Raja Casablanca ya Morocco.

Kwa wakati huo, mechi ya kwanza tu Yanga ilichapwa mabao 6-0 na Raja Casablanca, ikachapwa 3-0 na ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Uhuru kisha ikaenda Afrika Kusini kupambana na Manning Rangers na kuambulia kichapo kingine cha mabao 4-0. Baada ya hapo ikapoteza ugenini 2-1 dhidi ya ASEC Mimosas, 1-1 na Manning kisha sare ya mabao 3-3 na Raja Casabalanca kwenye Uwanja wa Uhuru na kumaliza michezo sita ya hatua ya makundi ikiwa imefunga mabao matano tu na kuruhusu 19.

Gamondi aliyewahi kufundisha timu mbalimbali alifika hatua hiyo ya makundi baada ya miaka hiyo 25 kufuatia kuifunga Al

Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo kwani awali ilikuwa haijawahi kushinda.

Yanga ilikuwa haijawahi kuifunga Al Merrikh katika mechi za CAF ila chini ya Gamondi timu hiyo ya Sudan ilipoteza mabao 2-0, Septemba 16, 2023 yaliyofungwa na Kennedy Musonda na Clement Mzize ikiwa uwanja wake wa nyumbani jijini Rwanda.

Mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Septemba 30, 2023, lililofungwa na Clement Mzize lililoiwezesha kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 3-0.

Ushindi wa mabao 4-0, ilioupata Yanga dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria Februari 24, 2024, katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ulimfanya Gamondi kuandika rekodi mpya ya kuivusha robo fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia yao.

Kwa mara ya kwanza Yanga iliwahi kucheza hatua ya robo fainali enzi hizo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970 na kucheza makundi 1998 ila tangu hapo haikuwa na maajabu hadi msimu wa 2022-2023, ilipotinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Pia iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na 2018 huku ikifika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika 1995.

Msimu uliopita ambao Yanga ilifika hatua ya robo fainali na kuishia hapo ilitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa kupoteza kwa mikwaju ya penalti 3-2, baada ya miamba hiyo kutoka suluhu michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.

Kama sio mwamuzi kufumba macho na kulikataa bao la Stephane Aziz KI katika mechi dhidi ya Mamelodi kukle Afrika Kusini, huenda habari ingekuwa nyingine na Yanga ingetinga nusu fainali na kufikia reklodi iliwahi kuweka na Simba tu mwaka 1974 wakati michuano hiyo ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika.

Sio hivyo tu, Gamondi anaondoka akiwa ni kocha pekee wa Yanga aliyewahi kuiingiza timu hiyo mara mbili mfululizo hatua ya makundi, kwani haikuwahi kuyokea kabla ya hapo baada ya kugawa dozi za maana kwa Vital’O ya Burundi na CBE ya Ethiopia akifunga jumla ya mabao 17-0. Rekodi tamu zaidi ni Yanga kwa mara ya kwanza katika historia yake kuoata ushindi kwenye ardhi ya Ethiopia dhidi ya timu za nchi hiyo kwani kwa miaka mingi ya michuano ya CAF ilikuwa ikiitaaabika hata kama ikishinda nyumbani, kule iliishia kunyukwa au kutyoka sare tu, lakini kwa Gamondi iliwezekana.

Na kwa sasa ni kwamba timu imetinga hatua hiyo kwa mara ya pili na sasa timu inasubiri kuanza mbio za kuitafauta robo fainali ikipangwa Kundi A sambamba na Al Hilal ya Sudan, TP Mazembe ya DR Congo na MC Alger ya Algeria ambazo zote imeshawahi kukutana anazo katika mechi za michuano ya CAF kwa misimu tofauti.

Gamondi aliandika rekodi nyingine mpya ya kibabe kwa kuifanya Yanga iwe ya kwanza nchini kushinda mabao mengi zaidi kwa timu za Kaskazini.

Ushindi huo wa mabao 4-0, dhidi ya CR Belouizdad uliifanya kuivuka rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019 ambapo ilikuwa ya kwanza nchini kuifunga JS Saoura ya Algeria kichapo cha mabao 3-0.

Mabao ya Simba yalifungwa na nyota wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere aliyefunga mawili na kuifanya kumaliza nafasi ya pili katika kundi lake la ‘D’ na pointi tisa nyuma ya vinara Al Ahly ya Misri iliyomaliza na pointi 10.

Moja ya jambo kubwa litakalokumbukwa kwa Gamondi ni kuiwezesha timu hiyo kushinda kwa mabao 5-1, dhidi ya Simba Novemba 5, 2023, yaliyofungwa na mastaa, Kennedy Musonda, Stephane Aziz KI na Pacome Zouzoua huku Maxi Nzengeli akifunga mawili.

Simba ilikuwa haijawahi kufungwa na Yanga idadi kama hiyo kubwa ya mabao tangu ilipolazwa 5-0 mwaka 1968, kipigo ambacho Simba ilikilipa kwa kishindo mwaka 1977 kwa kuifumua Yanga 6-0 kisha kupigilia msumari mwingine wa mabao 5-0 mwaka 2012.

Kichapo hicho kilimfukuzisha kazi Kocha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ambaye alikuwa na rekodi nzuri mbele ya Yanga akiifunga mara tatu kwenye mechi tofauti ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii, japo mambo yote yalibadilika.

Tangu aingie madarakani kuiongoza timu hiyo, Gamondi amesajili nyota wapya 18 kutoka klabu mbalimbali akianza na Nickson Kibabage (Singida Fountain Gate), Gift Fred (SC Villa), Jonas Mkude (Simba) na Maxi Mpia Nzengeli (AS Maniema Union).

Wengine ni Kouassi Yao, Pacome Zouzoua (ASEC Mimosas), Mahlatse Makudubela (Marumo Gallants), Hafiz Konkoni (Bechem United), Shekhan Ibrahim Khamis (JKU), Augustine Okrah (Bechem United) na Joseph Guede Gnadou kutoka Tuzlaspor FC.

Kwa msimu huu, nyota wapya ni Clatous Chota Chama (Simba), Prince Dube, (Azam FC), Chadrack Boka (FC Lupopo), Khomeiny Abubakar, Duke Abuya (Singida Black Stars), Aziz Andambwile (Fountain Gate FC) na Jean Baleke (Al-Ittihad SCS Tripoli).

Related Posts