Wananchi waombwa maoni ujio wa Starlink Tanzania

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tangazo la kukaribisha maoni ya wananchi kuhusu maombi ya leseni ya kampuni ya Starlink inayotoa huduma za mawasiliano ya intaneti.

Hatua hiyo inaashiria kuwa Starlink ambayo inamiliki na bilionea namba moja duniani, Elon Musk, huenda ikaanza kutoa huduma hapa nchini endapo wananchi wataridhia ipewe leseni.

Hapo awali, Elon Musk alieleza kuwa uzinduzi wa huduma hiyo nchini Tanzania uliotakiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka 2023, ulisogezwa mbele kutokana na changamoto za kupata vibali vinavyohitajika.

Tangazo la TCRA lililotolewa leo Novemba 15, 2024 limeeleza kuwa Starlink Satellite Tanzania Limited ni miongoni mwa kampuni zilizoomba leseni chini ya mfumo wa leseni shirikishi. Mamlaka hiyo imeweka kipindi cha siku 14 kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Aidha, mazungumzo ya muda mrefu kati ya Starlink na Serikali ya Tanzania yalihusu haki za masafa ya mawasiliano na namna ya kufuata sheria za ulinzi wa data.

Muda wote Serikali ilisisitiza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa muhimu katika kuhakikisha huduma hiyo inazingatia mahitaji ya ndani.

Starlink, inayomilikiwa na kampuni ya SpaceX, ilianza kutoa huduma zake katika soko la Afrika Mashariki mwaka jana, ambapo Kenya na Rwanda zilianza kupata huduma zake za intaneti ya kasi kupitia satelaiti zenye nguvu zaidi duniani.

Related Posts