Mathayo Gekul mwenyekiti mpya Chadema Manyara

Babati. Aliyekuwa mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Babati Vijiji mwaka 2020, Mathayo Gekul amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Manyara.

Gekul ambaye ni mdogo wake mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul ameibuka kidedea kwenye kinyang’anyiro hicho, kilichohusisha wagombea watatu wakiwania kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Derick Magoma ambaye hakugombea.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema ndiye amesimamia uchaguzi wa Chadema Mkoa wa Manyara, kuwapata viongozi wapya watakaotumikia nafasi hizo kwa miaka mitano ijayo na kumalizika usiku wa Novemba 14, 2024.

Mathayo ambaye aliwahi kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Vijana Taifa (Bavicha) mwaka 2021, ameshinda nafasi hiyo akiwabwaga wenzake kwa kishindo.

Akitangaza matokeo hayo mjini Babati, Lema amesema Mathayo amepata kura 45, huku Leonard Mao akipata kura tano na Emmanuel Landey kura tisa.

Amesema nafasi ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Manyara, amemshindi ni  Gervas Sulle aliyepata kura 44 huku wenzake Daniel Tango akipata kura sifuri, Omari Bakari (4) na Gabriel Boay kura 12.

Lema amesema Regula Mtei amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha) na Josephine John Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) wa Mkoa wa Manyara.

Akizungumza na wajumbe wa kikao hicho, Lema ameeleza kutofurahia namna mchakato ulivyokwenda wa kupitisha wagombea kwani kuna maeneo umefanyika uhuni na baadhi ya watu kuanzisha vurugu.

“Hao waliofanya huo uhuni, nendeni mkawaambie, mtu na mkwe wake kuwa watalipia kwa hili, kwa kuwa mchezo mchafu umefanyika maeneo mengi,” amesema Lema.

Kwa upande wake, Mathayo amewashukuru wajumbe wa kikao hicho kwa kumchagua kushika nafasi hiyo na amewataka viongozi wenzake wa mkoa huo, wilaya na ngazi za msingi kusimama imara katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amewataka kutoa ushirikiano kila mahali ambapo Chadema imeweka wagombea.

Related Posts